Ojuku Abraham, Amani
DAR ES SALAAM: Leo ni siku ya 70
tangu Miss Tanzania Mwaka 1996, Shose Mori Sinare aanze kusota lupango
katika Gereza la Ukonga jijini Dar akikabiliwa na mashtaka katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, maisha yake yaanikwa na Amani linakupa zaidi.
TUHUMA ZAKE
Shose, aliyekuwa mkurugenzi kwenye Benki
ya Stanbic, anashtakiwa pamoja na wengine wawili, kamishna mkuu wa
zamani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na Sioi Graham
Solomon aliyekuwa ofisa mwandamizi wa zamani wa taasisi hiyo ya fedha.
ANAVYOHENYA
Katika siku zote hizo, Shose amekuwa
akihenya kupata dhamana, lakini inashindikana kutokana na kuwepo kwa
kosa la utakatishaji fedha, ambalo kisheria halina dhamana.
Licha ya kosa hilo la utakatishaji
fedha, mashtaka mengine yanayomkabili Shose ni pamoja na kudaiwa
kuwasilisha nyaraka za uongo kwa lengo la kujipatia fedha, kujipatia
fedha kwa njia za udanganyifu, makosa ambayo yote anadaiwa kuyafanya
alipokuwa mfanyakazi wa benki hiyo ambapo nyakati tofauti, wote
wanatuhumiwa kujipatia kiasi cha dola milioni 6 (sawa na shilingi
bilioni 13) kutokana na mkopo wa serikali ya Tanzania kutoka Benki ya
Standard ya Uingereza wa dola milioni 600 (sawa na shilingi trilioni
1.3).
CHANZO KUTOKA GEREZANI
Kwa mujibu wa chanzo chetu kutoka gereza alipo Shose, amekuwa akisali usiku na mchana kumwomba Mungu awe upande wake.
“Kinachomuumiza sana ni ile nenda rudi
ya mahakamani. Yeye hakuzoea misukosuko. Kwa hiyo anahisi
kuchanganyikiwa na hali hiyo inampa tabu sana.
“Wakati mwingine anashangaa kuona kama
siku haziendi vile, si unajua mambo ya kesi. Kwa kweli uchangamfu wake
ni wa usoni tu lakini ndani ya moyo anaumia sana yule mrembo.
“Ila naweza kusema kwamba, ndugu zake
wanampa sapoti kubwa kwani huwa wanakuja kumuona. Kilio chake kikubwa
Shose ni kupata dhamana, hilo ndilo analoliombea kwa Mungu. Lakini
vinginevyo ni mdada mtulivu sana, si mwongeaji akiwa mahabusu na
wenzake. Anaonekana ana akili sana.
“Siku moja nilimuuliza anajisikiaje kuwa
mahabusu akasema ni changamoto za maisha ambazo binadamu hupitia, siku
za mwanzo, yaani ile siku ya kwanza, ya pili na ya tatu, zilikuwa ngumu
sana kwake, lakini baadaye akakubaliana na hali halisi,” kilisema chanzo
hicho.
WAREMBO WAMWOMBEA
Baadhi ya washiriki na washindi
waliopata kutwaa taji hilo kwa miaka tofauti, walimuombea kwa Mungu,
Shose ili kesi hiyo yenye ushindani mkubwa wa kisheria, iweze
kumalizika salama kwa upande wake.
“Dunia ina mapito mengi na hii yote ni
mitihani ambayo mwisho wa siku tunamtegemea Mungu kuweza kushinda. Kesi
ni kesi, lolote linaweza kutokea, lakini Mungu ni mkubwa, tunamuombea,”
alisema mshiriki wa Miss Tanzania 2001, Rashida Wanjara…
Naye Miss Tanzania 1999, Hoyce Temu kwa upande wake, alisema amekuwa akimwombea kwa Mungu mrembo huyo kuhusu kesi yake.
“Najua ishu ipo mahakamani na bado
hukumu haijapita. Kwa hiyo ni mtuhumiwa tu hajapatikana na hatia.
Watanzania tumwombee Shose (pichani) kwani yaliyompata ni changamoto za
dunia kama mwanadamu,” alisema Hoyce.
TUJIKUMBUSHE
Shose aliyeshinda taji hilo akichukua
mikoba ya Emily Adolf, alikuwa mlimbwende aliyetoa matumaini makubwa ya
kushinda Miss World, hasa kutokana na uwezo wake mkubwa katika lugha ya
Kiingereza, ambayo wakati huo ilionekana kuwa tatizo lililowaangusha
watangulizi wake.
Hata hivyo, kama walivyokuwa washindi
wote wa taji la Miss Tanzania, ukimuondoa Nancy Sumari walioshiriki
shindano la dunia, Shose hakufanya vizuri kwenye michuano hiyo ambayo
mwaka huo ilifanyika Bangalore, nchini India na Miss Ugiriki, Irene
Skliva kutwaa taji.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini