Watu
wawili wamefariki dunia na wengine 36 kujeruhiwa, kati yao wanne vibaya
baàda ya basi walilokuwa wakisafiria kutokea jijini Dar es Salaam
kuelekea Morogoro, mali ya kampuni ya BM kuligonga ubavuni lori
lililokuwa likija mbele yake na kuangukia kwenye bonde pembeni ya
barabara na kupinduka mara nne, katika eneo la Lubungo Mikese, barabara
kuu ya Morogoro-Dar es Salaam.
ITV imefika katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Morogoro na
kushudia majeruhi wa basi hilo la kampuni ya BM wakiletwa kwa magari
binafsi na basi jingine la kampuni hiyo, wakionekana kujeruhiwa zaidi
maeneo ya kichwani, usoni na miguuni, ambapo mwandishi alilazimika
kuweka kalamu pembeni na kusaidiana na wananchi wengine kuwabeba
majeruhi na kuwaingiza kwa madaktari kupata huduma ya kwanza,huku
vitanda vya kuwabebea vikionekana kuwa vichache ikilinganishwa na wingi
wa majeruhi, ambapo baadhi ya waliohojiwa wameeleza namna ajali hiyo
ilivyotokea na kulalamikia wizi uliofanywa na waliofika eneo la tukio
baada ya ajali.
Daktari bingwa wa upasuaji katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa
Morogoro, Francis Semwene amekiti kupokea miili ya wanaume wawili na
majeruhi 36, ambapo wanne kati yao hali zao ni mbaya na wengine
italazimika kuwakata baadhi ya viungo iwapo watashindikana kushonwa.
Kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro Leonard Paulo akizungumzia ajali
hiyo, amesema chanzo ni mwendo kasi na imetokea majira ya saa 3:30
usiku ikihuhusisha basi la mwisho kutoka jijini Dar es Salaam kuja
Morogoro, mali ya kampuni ya BM, baada ya dereva wake kufika Lubungo
eneo lenye kona na mteremko mkali, na akiwa mwendo kasi, kukutana mbele
na lori likiwa na tela, likitokea uelekeo wa Morogoro kuelekea Dar es
Salaam, likiwa linamalizia kupita lori jingine lililokuwa limeegesha
barabarani baàda ya kuharibika, ambapo dereva wa basi aligonga tela la
lori hilo lililokuwa kwenye mwendo na kukosa uelekeo na kupindukia
bondeni na kusababisha vifo na majeruhi hao.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini