Mtu mmoja ameuawa na tembo wengine kadhaa wamejeruhiwa katika
mapambano kati ya wananchi na kundi la tembo yaliyotokea katika kijiji
cha kitendeni kata ya Irkaswa tarafa ya Endyment wilayani Longido mkoa
wa Arusha.
Mkuu wa Wilaya ya Longido Bw.Ernest Kahindi amesema katika
mapambano hayo pia tembo mmoja ameuawa na wengine sita wamejeruhiwa na
kwamba hali katika eneo hilo sio shwari na huenda kukawa na madhara
makubwa zaidi.
Akizungumza wakati anaelekea katika eneo la mapambano hayo
yanayodaiwa kuanza mapema alfajiri Bw.kahindi amesema hatua za awali za
kutuliza hali hiyo zilikuwa zinaendelea kwa ushirikano wa viongozi wa
ngazi mbalimbali na watendaji wa idara za wanyamapori zikiwemo za
kuwaondoa tembo hao katika eneo hilo zoezi ambalo licha ya kuwa gumu
lilikuwa linaendelea vizuri.
Aidha Bw.Kahindi amesema tofauti kati ya tembo hao na wananchi
ilijitokeza baada ya wanyama hao kumuua kijana mmoja wa jamii ya
kifugaji na ndipo wananchi hao wakajikusanya na kuanza kuwatafuta tembo
hao na kuanza kupambana nao kutaka kulipiza kisasi ambapo pia mwananchi
mwingine mmoja amejeruhiwa vibaya na tembo zaidi ya sita pia
wamejerihiwa vibaya kwa kuchomwa mikuki na kupigwa kwa silaha zingine
za jadi.
Hata hivyo Bw.Kahindi ambaye ameambatana na kamati ya ulinzi na
usalama ya wilaya kuelekea eneo la tukio amesema taarifa kamili ya
tukio hilo na hatua zitakazochukuliwa itatolewa baadaye japo ameendelea
kuwaomba wananchi kuepuka kuchukua sheria mkononi ikiwemo ya kuamua
kupambana na wanyama ili kuepusha madhara zaidi kutokea.
Asilimia kubwa ya eneo hilo ambalo ni mapito ya wanyama kwa muda
mrefu sasa limekuwa katika hekaheka kati ya wananchi na wanyama hao
hasa unapotekea uharibifu ukiwemo wa wanyama kula mifugo ya wananchi ama
kuua watu.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini