Waziri Maghembe Afichua Siri Ya Uteuzi Wa Jenerali Gaudence Milanzi Wizara Ya Maliasili. | nyula blog

Habari Kila Pande

Breaking News
Loading...

Sunday, January 3, 2016

Waziri Maghembe Afichua Siri Ya Uteuzi Wa Jenerali Gaudence Milanzi Wizara Ya Maliasili.


Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe amefichua sababu za Rais John Magufuli, kumteua Meja Jenerali Gaudence Milanzi kuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo.

Profesa Maghembe alisema lengo ni kuwa na kamanda atakayeongoza mapambano dhidi ya ujangili na kutoa onyo kwa majangili kujisalimisha na silaha zao, vinginevyo watakiona cha mtema kuni.

“Yale maneno maneno kuwa majangili watakimbilia kujificha msituni au kwenye makorongo wajue tutawafikia tu. Tumejiandaa kikamilifu hata kama wataingia makaburini kujificha tutawafikia,” alisema.

Profesa Maghembe alitoa kauli hiyo juzi wilayani Mwanga baada ya kupokewa na wanachama na viongozi wa CCM alipowasili jimboni humo.

“Kwa kweli kiama chao kimefika na tutapambana kisayansi na hata uteuzi wa mheshimiwa Rais jana (Alhamisi) wa Meja Jenerali Milanzi ni kuwa na kamanda atakayeongoza mapambano,” alisema.

Waziri huyo alisema Desemba 30, mwaka jana alikutana na Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa) na kuweka mikakati kabambe ya kutokomeza ujangili na majangili.

“Jana (Desemba 30) niliwaita na kukaa nao kwa saa nne kupanga mikakati ambayo ni siri, lakini ujue mamlaka hiyo ina watu mashuhuri sana wamo wanajeshi humo. Tumejipanga hatutanii,” alisema.

Bodi hiyo iliyoteuliwa na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, Septemba mwaka jana inaongozwa na Meja Jenerali mstaafu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Hamis Semfuko.

Wajumbe wengine wa bodi hiyo ni pamoja na Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Meja Jenerali Samwel Ndomba na Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Abdulrahman Kaniki.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini

google+

linkedin