Naibu
Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani ametoa siku 14 kwa
mgodi wa dhahabu wa Buckreef kuanza uzalishaji ama sivyo wataandikiwa
hati ya makosa na Afisa Madini Mkazi katika mkoa wa Geita.
Naibu
Waziri alitoa agizo hilo baada ya kufika katika mgodi huo uliopo
katika kata ya Lwamgasa mkoani Geita na kuona hakuna shughuli zozote za
uzalishaji zinazoendelea.
“Najua
kuwa hamjazalisha dhahabu mpaka sasa, lakini lazima mzalishe ili kulipa
kodi na mrabaha, bila kufanya hivyo ndani ya siku 14 zijazo mtaandikiwa
hati ya makosa kama sheria ya madini ya mwaka 2010 inavyoelekeza, mgodi
huu mnaumiliki toka mwaka 2011, lazima muanze uzalishaji,” alisema
Kalemani.
Aidha
Naibu Waziri alisema kuwa mgodi huo umechukua maeneo makubwa ya
uchimbaji madini lakini hawayatumii, hivyo wayaainishe maeneo
wanayohitaji kutumia na mengine wapewe wachimbaji wadogo.
Akijibu
suala la ugawaji wa maeneo kwa wachimbaji wadogo, Mkurugenzi Mtendaji
wa kampuni ya Tanzam2000 inayomiliki mgodi huo kwa ubia na Shirika la
Madini la Taifa (STAMICO), Joseph Kahama alisema kuwa wako tayari kukaa
na Ofisi ya Madini mkoani Geita na STAMICO ili kuainisha maeneo
watakayowaachia wachimbaji wadogo.
Kutokana
na hilo Naibu Waziri alimwagiza Afisa Madini Mkazi mkoa wa Geita,
Mhandisi Laurian Rwebembera kukaa na watendaji wa mgodi huo tarehe 10
mwezi huu ili kuainisha maeneo hayo na kisha wayagawe kwa wachimbaji
wadogo.
Awali
akizungumza na wachimbaji wadogo katika kijiji cha Lwamgasa, Dkt.
Kalemani aliwaeleza kuwa serikali imeongeza kiwago cha utoaji wa ruzuku
kutoka Dola za Marekani 50,000 hadi Dola Laki Moja kwa kikundi na
kuwaasa wachimbaji hao kujiunga katika vikundi ili kuweza kuwa na sifa
ya kupata ruzuku hizo.
“Tunataka
ruzuku hizi ziwafaidishe wananchi wengi lakini si mtu mmoja mmoja,
ruzuku iwasaidie katika shughuli za uchimbaji madini ikiwemo kununua
vifaa vya uchimbaji lakini na ninyi lazima mlipe kodi,” alisema Naibu
Waziri.
Aidha
Mkuu wa mkoa wa Geita, Fatma Mwasa alimweleza Naibu Waziri kuwa maeneo
yanayotengwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo ni vyema yakawa yanafanyiwa
utafiti ili kuhakikisha kama yana madini na hivyo kuepusha wachimbaji
hao kuwekeza katika maeneo yasiyo na madini.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini