Mkuu
wa wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Bi.Hawa Ng'humbi amewaagiza wakuu
wa idara katika halmashauri ya wilaya hiyo pamoja na watendaji wa kata
na vijiji kuhakikisha watu wote watakaowapa mimba wanafunzi wanasakwa na
kufikishwa mahakamani mara moja kwakuwa vitendo hivyo vimekuwa
vikiongezeka siku baada ya siku wilayani humo hali inayorudisha nyuma
jitihada za kukuza kiwango cha elimu nchini.
Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya
Idukilo wilayani Kishapu Shinyanga baadhi ya wananchi wamemtaka mkuu wa
wilaya ya Kishapu Bi.Hawa Ng'humbi kufuatilia kwa karibu zaidi swala la
mimba na ndoa za utotoni ambazo zimekua kero inayodumaza elimu katika
kata hiyo huku baadhi ya wazazi wakiendelea kuwaozesha watoto wakike
wakati wakiwa wadogo kwa lengo la kujipatia mali.
Awali katika mkutano huo mkurugenzi wa shirika la Agape
linaloshughulika na haki za watoto wa kike Bw.John Myola amedai kuwa
rushwa iliyokithiri kwa watumishi wa serikali imekuwa chanzo kikubwa cha
mimba na ndoa za utotoni hali ambayo isipodhibitiwa mapema taifa
litaendelea kupoteza nguvu kazi kwa ongezeko la vifo vya wanawake na
watoto wachanga wakati wa kujifungua.
Akitoa maagizo kwa wakuu wa idara, watendaji wa kata na vijiji
pamoja na wazazi Bi Hawa Ng'humbi amesema yeyote atakayebainika kumpa
mimba mtoto wa kike afikishwe mahakamani maramoja ili hatua za kisheria
zichukuliwe huku akilipongeza shirika la Agape kwa jitihada kubwa za
kumkomboa mtoto wakike ambapo alipokea vyerehani vitano kutoka shirika
hilo na kuwakabidhi baadhi ya wasichana waliokuwa wamekatizwa masomo yao
baada ya kupata mimba na kuacha masomo yao.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini