TAMKO LA ASASI ZA KIRAIA TANZANIA (AZAKI) KUHUSU HALI YA KISIASA VISIWANI ZANZIBAR 10/1/2016
________________________________________
________________________________________
Sisi
wana Asasi za Kiraia nchini - AZAKI, tulikutana tarehe 17 Novemba 2015,
ambapo ni zaidi ya wiki tatu baada ya uchaguzi mkuu kumalizika na
kutathimini mwenendo wa uchaguzi mkuu na hali ya kisisasa visiwani
Zanzibar.
Baada
ya tathmini yetu ya kina kama AZAKI tulitoa tamko na kuwataka wanasiasa
kufanya mambo kadhaa ili kuinusuru Zanzibar na hali ya machafuko.
Kati ya mambo tuliyowataka wanasiasa kuyazingatia ili kuendeleza amani na utengamano nchini ni pamoja na:
1.
Uwepo utaratibu wa kutolewa taarifa ya maendeleo ya majadiliano
yanayofanywa na viongozi wanaokutana kuhusu suala la muafaka wa kisiasa
Zanzibar, ikieleza lengo la majadiliano na muda wake; ikumbukwe
kikatiba, wananchi wana haki ya kujua na kushirikishwa katika masuala
yoyote yanayohusu maslahi yao na nchi yao.
2.
Wakati majadiliano yakiendelea, (i) Vyombo vya ulinzi na usalama
viendelee kuwalinda wananchi kwa mujibu wa sheria za nchi na kusiwe na
utaratibu wa kuwanyanyasa kama inavyolalamikiwa na baadhi ya watu kuhusu
manyanyaso yanayofanywa na wanausalama
3.
Tuliwataka viongozi wanaojadiliana na wadau wengine wote wenye mchango
katika kuiona Zanzibar inaishi kwa amani na salama, wajikite sana katika
kuzingatia sheria na katiba wanapokusudia kufanya maamuzi ya utatuzi wa
mgogoro wa kisiasa Zanzibar, kwa sababu kinyume na hivyo, watazua
machafuko kwa kufikia maamuzi yasiyofuata au yanayokinzana na sheria na
katiba.
Kila mtu anawajibika kutii misingi ya sheria na katiba na pia masuala hayo ni muhimu katika kuepusha migongano na machafuko.
Baada
ya Tamko hili AZAKI tumeendelea kufuatilia hali ya kisiasa Zanzibar.
Tumefanya hivyo tukiamini kuwa uchaguzi ni sehemu muhimu ya michakato ya
kidemokrasia hapa nchini kama ilivyo duniani kote.
Sisi
asasi za kiraia Tanzania, tukiwa watetezi na wasimamizi wa demokrasia,
utawala bora na haki za binadamu, hatuegemei upande wa mgombea yeyote
wala chama chochote cha siasa kinachotafuta kuingia madarakani wala
hatulengi kuchukua dola bali tunataka haki itendeke Visiwani Zanzibar.
Aidha,
AZAKI tunasikitishwa na hali isiyoridhisha ya kisiasa Visiwani humo
ambayo imetokana na kufutwa kwa uchaguzi kwa sababu zisizokuwa na tija
kwa taifa , uliofanyika tarehe 25 Oktoba 2015.
Tunaona
kumeibuka mgogoro mkubwa wa kisiasa kufuatia uamuzi wa Mwenyekiti wa
Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Bw. Jecha Salim Jecha wa kufuta
uchaguzi mkuu wote wa Zanzibar, kwa maana ya uchaguzi wa kumchagua Rais,
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani wa Zanzibar.
Tathmini
yetu kama AZAKI tuliona uamuzi huo wa kufuta uchaguzi haukuwa sahihi
kisheria na haukubaliki kwa sababu umevunja katiba na kwamba umefanywa
kwa msukomo wa maslahi binafsi ya kisiasa kwa kuwa si Mwenyekiti wala
Tume ya Uchaguzi yenye mamlaka ya kisheria ya kufuta uchaguzi.
Kwa
ufupi, hakuna kifungu chochote cha sheria wala Katiba ya Zanzibar ya
1984 kama ilivyorekebishwa mwaka 2010 kinachompa uwezo Mwenyekiti au
Tume kuchukua uamuzi kama huo.
Uamuzi
huo umezusha mtafaruku mkubwa huko Zanzibar na Tanzania kwa ujumla,
umeibua malumbano na mivutano katika jamii na hiyo kwenda mbali zaidi
kwa kuibua upya mvutano wa kisiasa kati ya vyama vikuu viwili vya siasa
vya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF).
Hali ya Sasa ya Mazungungumzo
Huku
tukitambua kwamba kukutana na kujadiliana kwa viongozi wa ngazi ya juu,
wakiwemo marais wastaafu wa Zanzibar, ni njia muafaka ya kutafuta
suluhu ya mgogoro, tunataka ieleweke wazi kuwa vikao visivyokuwa na
mwisho wala taarifa inayotolewa kwa umma kuhusu maendeleo yake, havileti
matumaini kwa wananchi.
Ni
haki ya msingi na ya kikatiba kwa wananchi kupewa taarifa ya maendeleo
ya vikao hivyo; waelezwe vinalenga nini; na kwa muda gani viongozi
wanaweza kumaliza majadiliano.
Kwa
mujibu wa Ibara ya 18 (2) ya Katiba ya Zanzibar ya 1984 kila raia anayo
haki ya kupewa taarifa na kujua yote yote yale yahusuyo mustakabali wa
taifa na maisha yake.
AZAKI
tumebaini Mazungumzo ya viongozi wakuu yanafanyika katika hali ya usiri
mkubwa na lililo baya zaidi hakuna utaratibu wa wananchi kupewa taarifa
fafanuzi ya maendeleo ya mazungumzo hayo.
Huku
wanasiasa wa vyama hivo viwili wakisikika kutoa kauli zinazogonganisha
wananchi na kuwachanganya. Matokeo yake kujenga hofu inayoumiza mioyo ya
wananchi.
Wananchi
wananyimwa haki yao ya kujua masuala yanayohusu mustakabali wa nchi yao
hasa pale inapoonekana wazi walishiriki kupiga kura ya kuchagua
viongozi wanaowataka.
Hili limethibitishwa na asasi za kiraia za uangalizi wa uchaguzi za ndani ya nchi na hata waangalizi wa kimataifa.
Hofu
kubwa tuliyonayo sisi wana Asasi za Kiraia ni kwamba kuendelea kwa
ukimya mkubwa kunaongeza minong'ono katika jamii, hali inayoweza kuzusha
migongano na kusababisha haki na amani kuchezewa na wasiokuwa na nia
njema ya kuiona Zanzibar inaishi katika amani na kuendeleza utengamano
kutokana na kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Kwa
sasa kuna hali ya utata kuhusu uongozi uliopo madarakani Zanzibar
kutokana na sababu mbalimbali za kisheria tulizoeleza katika tamko letu
la awali.
Kwa
mujibu wa Ibara ya 21 (1) ya Katiba ya Zanzibar ya 1984 ( kama
ilivyoboreshwa mwaka 2010) kila Mzanzibari anayo haki ya kushiriki
katika shuguli za utawala kwa kupitia wawakilishi waliowachagua
wenyewe.
Katika
mazingira ya uongozi wa Zanzibar yaliyopo kwa sasa, ni wazi kuwa nchi
inaendeshwa kwa muda mrefu bila ya kuwepo chombo cha kutunga sheria na
cha uwakilishi ambacho ni muhimili muhimu katika uendeshaji wa
serikali.
Katiba
ya Zanzibar Ibara ya 90(1) imeruhusu hali ya kuendesha nchi bila ya BLW
kwa muda usiozidi Siku Tisini (90) kuanzia Baraza lilipovunjwa.
Kipindi
hicho kikatiba kilikwisha toka tarehe 12 Novemba 2015, kwa kuwa Baraza
lilivunjwa rasmi tarehe 13 Agosti 2015. Itakapofikia January 12/2016
itakuwa ni miezi miwili ziadi Zanzibar kuendeshwa bila uwepo wa Baraza
la wawakilishi, kitu ambacho ni kinyume na Katiba.
Wito Wetu
1.
Muungano wa Asasi za Kiraia Tz (AZAKI) tunatambua hatua busara za
viongozi kutambua wajibu wao na kukutana kujadili njia ya kuondoa
mgogoro.
Tunadhani
viongozi wamepata muda wa kutosha kujadiliana na sasa ni imani yetu
kuwa wakati umefika kwa viongozi wanaokutana kutoka hadharani ikiwezekan
siku ya maazimisho ya Mapinduzi ya Zanzibar, tena kwa pamoja, na kutoa
taarifa fafanuzi inayojibu yafuatayo:
Ajenda
zao ni zipi? Wamefikia wapi? Wamebakiza wapi? Ni lini watamaliza
majadiliano? Lini watatoa tamko la MUAFAKA wa kumaliza mgogoro?
2.
Ni msimamo wa AZAKI kwamba katika hali yoyote ile, ni muhimu sana
utatuzi wa mgogoro uwe unaozingati msingi wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka
1984, Toleo la Mwaka 2010 pamoja na Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar Na.
11 ya mwaka 1984.
Tunasisitiza
hili kwa kuamini kuwa upatikane uamuzi ambao utakubalika kisheria kwa
maana ya kuwa hautafikiriwa kuhojiwa mbele ya sheria.
3.
Tunawataka viongozi wote watumie siku ya Mapinduzi ya Zanzibar
kuwatangazia wananchi hatma ya Zanzibar kisiasa, kwa kuwa Mzanzibari
anayohaki na uhuru wa kushiriki kwa ukamilifu katika uamuzi juu ya mambo
yanamhusu yeye na Taifa lake.
Wananchi
walishiriki kwa kupiga kura na sasa wanakila sababu ya kujua hatma ya
viongozi waliowachagua. Haki hii ni ya kikatiba kwa mujibu wa Ibara ya
21 (2) ya Katiba ya Zanzibar, na inaweza kwenda kudaiwa mahakamani muda
wowote.
4.
Tunawasihi viongozi wote wa dini mbalimbali na wadau wa maendeleo
kuingilia kati suala la Zanzibar kwani viashiria vya viongozi wakubwa
kujibizana majukwaani vinaweza kuendelea kujenga chuki miongoni mwa
jamii
5.
Pia tunawakumbusha vyama vya siasa vyote viamke na kushinikiza Serikali
ya Awamu ya Tano kulipatia ufumbuzi suala la Zanzibar ili wananchi
waweze kuendelea na shughuli zao za kila siku.
6.
Vile vile pande zinazohusika na mgogoro huu zijiepushe kutoa kauli za
kuwachanganya wananchi, bali ni vyema taarifa zinazotolewa ziwe sahihi
na zisiwe na mkanganyiko.
7.
Wananchi nao ni wadau muhimu sana katika mgogogoro huu, kwani kwa
mujibu wa katiba ya Zanzibar Ibaara ya 9 (2) inaeleza wazi kwamba “
Mamlaka ya kuendesha nchi ni ya wananchi wenyewewe ambapo nguvu na uwezo
wote wa Serikali kufuatana na Katiba utatoka kwa wananch wenyewe”.
Wananchi
walishiriki kupiga kura ili kupata Serikali itokanayo na mamlaka yao,
hivyo kitendo cha viongozi wachache kukataa uchaguzi na kutowapa taarifa
za msingi kuhusu mkwamo huu wa Kisiasa ni kuvunja katiba ya Zanzibar.
Kwa
hali hii tunatoa wito, wananchi washirikishwe na kupewa taarifa zote za
mkwamo huu wa kisiasa hatua kwa hatua. Hata hivyo tunapaswa kuwapongeza
kwa ustahimilvu mkubwa waliounyesha na tunawasihi waendelee kuwa
watulivu huku wakiendelea kudai haki yao na kutunza amani visiwani
Zanzibar.
Mwisho
Sisi
Asasi za Kiraia (AZAKI) za nchini Tanzania zilizoundwa na kutambulika
kisheria na zinazofanya kazi katika masuala mbalimbali ya kisheria,
kijamii, kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni.
Kwa
umoja wetu tunasimamia na kuhimiza utawala wa sheria na haki za
binadamu na masuala yote ya kimaendeleo ili kuhakikisha maisha ya
watanzania yanakuwa bora katika nyanja zote.
Kwa
sababu hiyo, tunajiona tukiwa na jukumu kubwa la kukemea na kuvitaka
vyombo husika kufanya kazi kwa mujibu wa sheria ili kuepuka uvunjifu wa
amani na hivyo kulinusuru Taifa letu.
Imetolewa kwa niaba ya AZAKI zote nchini na asasi miavuli zilizofanya Mkutano Jijijini Dar es Salaam Tarehe 10/1/2016
Kwa niaba ya Asasi zote, inaletwa kwenu na:
Ismail Suleiman
Katibu Mkuu- Baraza la Taifa la Asasi za Kiraia (NACONGO)
Onesmo Ole Ngurumwa
Mratibu wa Kitaifa- Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC)
Deus M Kibamba
Mwenyekiti -JUKWAA LA KATIBA TANZANIA
Martina Kabisama-Mratibu Taifa
Mtandao wa Mashirika ya Haki za Binadamu Kusini Mwa Afrika(SAHRINGON)
Stepheni Msechu
Mwakilishi- Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS)
Omary Said- Rais
Chama cha Wanasheria Zanzibar (ZLS)
Salma Said
Mwenyekiti -Jumuiya ya Waandishi za Maendeleo Zanzibar- WAHAMAZA
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini