Waziri
mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali imeamua kupambana na wala rushwa
ili kiasi kidogo cha rasilmali kilicholengwa kiweze kuwafikia wananchi.
Ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Watanzania waishio
Uingereza kwenye mkutano uliofanyika kwenye Ubalozi wa Tanzania jijini
London, Uingereza.
“Jambo tuliloamua kuanza nalo ni kupambana na rushwa. Tumeamua
kufanya hivyo ili kurudisha umoja na maelewano miongoni mwa Watanzania,
tunataka tuibadili Tanzania ili iwe ni ya Watanzania wote… tumechoka
kuambiwa sehemu fulani mradi umekamilika halafu ukienda kuangalia hukuti
kitu na fedha ile haipo,” alisema huku akishangiliwa.
Akizungumzia zoezi la kusaka watumishi hewa, Waziri Mkuu alisema
Serikali itawashughulikia wale wote waliohusika na zoezi hilo.
“Wafanyakazi hewa wamefikia zaidi ya 10,000 na tumeokoa zaidi ya sh.
bilioni 4.5 zilizokuwa zikipotea kila mwezi. Tukikamilisha zoezi la
kusaka watumishi hewa, sasa tutataka kujua ni akina nani walikuwa
wakipokea fedha hizo.
Waliohusika tutashughulika nao,” alisisitiza.
Alisema hivi sasa Serikali inalenga kuwa na watumishi ambao
wanafanya kazi kwa uaminifu, uadilifu na uwajibikaji mahali pa kazi.
“Hiki ndicho kipaumbele cha Serikali ya awamu ya tano na tena zoezi hili
litakuwa endelevu”, alisema Waziri Mkuu.
Akizungumzia kuhusu ukuaji wa uchumi, Waziri Mkuu ambaye alikuwa
London kuhudhuria mkutano uliojadili mapambano dhidi ya rushwa kwa niaba
ya Rais Dk. John Pombe Magufuli, alisema lengo la Serikali hivi sasa ni
kuona kuna ukuaji wa uchumi unaoenda sambamba na huduma zinazotolewa
kwa wananchi.
Alisema viwanda vingi viliuzwa na watu waliovinunua wakageuza kuwa
ni maghala ya kufugia wanyama. Sisi tunataka vifufuliwe ili teknolojia
mpya na za kisasa zije Tanzania. Nafasi ya kuwekeza iko kwa Watanzania
wote walioko nyumbani na ninyi mlioko nje,” alisema.
Alisema ardhi ipo ya kutosha na akawataka wawaalike marafiki zao
waje kuwekeza nchini, ili mradi wawe ni watu makini, wenye nia ya dhati
ya kuwekeza nchini na wenye mitaji na siyo madalali (middlemen).
“Tunataka usindikaji wa mazao na bidhaa ufanyike nchini mwetu badala ya
kupeleka mazao ghafi nje ya nchi, kwa njia hiyo tutakuwa pia tumezalisha
ajira kwa watu wetu,” alisema.
“Kuna Watanzania wanaishi Botswana, Ujerumani na Poland wameshaleta
wawekezaji nchini. Kwa mfano wa Poland wameleta mradi wa umeme katika
vijiji vitani wilayani Ileje. Kwa hiyo ninyi endeleeni kuishi Uingereza
lakini mhakikishe kuwa ukaaji wenu hapa, unaleta tija kule nyumbani.
Kumbukeni Tanzania na muwe tayari kuihudumia Tanzania,” alisema.
“Serikali inaamini itanufaika na uwepo wenu hapa Uingereza. Muweke
kipaumbele cha kuwekeza nyumbani na mkishindwa mtutafutie marafiki zenu.
Mwenye uwezo andaa andiko la mradi halafu uwasiliane na Balozi ili
akusaidie kutafuta wahusika kule nyumbani,” aliwaasa.
Akijibu swali kuwa ana maoni gani juu ya Bunge kutorushwa ‘LIVE’,
Waziri Mkuu alisema hatua hiyo ilichukuliwa ili kuwawezesha watu kufanya
kazi kama ambavyo kaulimbiu ya Mhe. Rais Magufuli ya Hapa Kazi Tu
inavyosema.
“Bunge la Tanzania lilikuwa ni bunge pekee katika Jumuiya ya Afrika
Mashariki na duniani ambalo lilikuwa likirushwa LIVE kuanzia asubuhi
hadi usiku. Ina maana katika kipindi cha Bunge la bajeti, ambalo
linaendeshwa kila siku kwa miezi mitatu, Watanzania nao wangekuwa LIVE
kwa miezi mitatu,” alisema.
“Tulilazimika kujifunza kutoka kwenye mabunge mengine. Hivi hapa
Uingereza mnaangalia Bunge live kila siku?” alihoji Waziri Mkuu na
kujibiwa kuwa linarushwa LIVE kwa pipindi kisichozidi dakika 15 wakati
wa maswali kwa Waziri Mkuu tu.
Akitoa ufafanuzi, aliwaeleza kwamba Bunge la Tanzania linarusha
‘LIVE’ kila siku asubuhi wakati wa maswali ya kawaida na Alhamisi
asubuhi wakati wa maswali kwa Waziri Mkuu lakini mijadala yote
hurekodiwa na kuhaririwa na kisha kurushwa kuanzia saa 8-9 mchana na saa
3-4 usiku kwa siku husika.
Kwa Watanzania wanaopenda kufanya kazi na wanapenda kufuatilia
mambo ya Bungeni, walikuwa hawaoni LIVE coverage jwa sababu walikuwa
kazini lakini sasa hivi wanaweza kufuatilia masuala ya bunge kwani muda
wa jioni uliopangwa mtu anakuwa ametoka kazini na anaweza kuangalia
televisheni akiwa nyumbani baada ya kutoka kazini.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini