WaziriMkuu
wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa, Kassim Majaliwa
amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi kufuatilia maendeleo ya
mradi wa umwagiliaji wa Narunyu katika kata ya Kiwalala wilayani Lindi.
Hatua hiyo imekuja baada ya wananchi wa kata hiyo kusimamisha
msafara wa Waziri Mkuu, Majaliwa katika eneo la Kiwalala jana na
kumuomba awasaidie kuhusu hatma ya mradi wao wa umwagiliaji ambao
walitakiwa wakabidhiwe tangu mwaka 2014.
Awali muwakilishi wa wananchi hao, Mohammed Bakar alisema kuwa
mradi huo uliogarimu shilingi milioni 600 ulitakiwa uwe tayari
umekabidhiwa kwa wananchi, lakini hadi sasa bado na hata banio
halijakamilika, hivyo wanashindwa kuendelea na kilimo katika eneo hilo.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu mradi huu bado haujaanza ila tulishangaa
wakati wa mbio za mwenge mwaka 2014 ilisomwa taarifa kwamba wakazi wa
Kiwalala wananufaika na mradi wa kilimo cha umwagiliaji wa Narunyu jambo
ambalo si kweli kwani mradi huu haujawahi kufanya kazi na hata banio
hakuna,” amesema.
Waziri Mkuu, Majaliwa amesema malalamiko hayo ya wananchi wa
Kiwalala lazima yafanyiwe kazi, hivyo amemuagiza mkuu wa mkoa wa Lindi,
Zambi kuhakikisha anakwenda kwenye kata hiyo kulipatia ufumbuzi suala
hilo.
“Kweli kuna miradi ambayo inaelekezwa na watu kwa viongozi kuwa
imekamilika wakati bado, namuagiza mkuu wa mkoa kulifanyia kazi jambo
hili,” amesema.
Pia amesisitiza kwamba serikali hii si ya kuleana, mtu
atakayebainika kukwamisha miradi ya maendeleo watamalizana naye hapo
hapo, hivyo aliwaomba wananchi kuwa na subira kwani taarifa yao
imepokelewa na inafanyiwa kazi.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini