Mkuu
wa Mkoa wa Arusha, Felix Ntibenda amesema idadi ya watumishi hewa
mkoani humo imeongezeka baada ya uchunguzi wa awali huku baadhi ya
waliokuwa wakifuja fedha za serikali kwa kudanganya wakiomba
kuzirejesha.
Aidha, amesema mkoa umepoteza Sh bilioni 1.8 kwa mwaka jana kutokana na kulipa watumishi hewa.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana mjini Arusha, Ntibenda alisema hivi sasa
mkoa huo unafuatilia akaunti za watumishi hao hewa ili fedha hizo
zirudishwe serikalini huku watumishi wengine baadhi waliokuwa wakifuja
fedha za serikali kwa kudanganya wakiomba kuzirejesha.
Alisema
awali wakati timu ya uchunguzi aliyoiunda kuchunguza watumishi hewa
ilibaini mkoa huo kuwa na watumishi hewa 270, lakini hadi jana idadi
hiyo imeongezeka na kufikia zaidi ya 300.
Alisema wilaya mbili za Karatu na Arumeru ndizo ambazo watumishi hewa wameongezeka.
“Bado
tunaendelea na uchunguzi na naamini wataongezeka lakini hivi sasa hao
watumishi hewa wanahaha kurudisha fedha za serikali lakini hata kama
wakirudisha watapelekwa mahakamani,” alisema Ntibenda.
Alisema
hata kama fedha hizo watazirudisha, lakini watawafikisha mahakamani na
pia wanafuatilia kujua ni kwa nini wakuu wa idara zao walifahamu udhaifu
huo, lakini walikaa kimya na kuwalipa mishahara huku wakijua kuwa
wanaihujumu serikali.
Alisisitiza
ni vyema watu wakaacha tabia ya kujipatia fedha nyingi kwa njia isiyo
halali kwani watumishi hewa wanasababisha fedha za serikali kushindwa
kufanya shughuli nyingine badala yake kupata hasara.
Katikati
ya mwezi uliopita, wakati akiwaapisha wakuu wa mikoa wapya, Rais John
Magufuli aliagiza waende kufuatilia watumishi hewa katika mikoa yao na
hadi sasa wamegundulika watumishi hewa zaidi ya 4,000.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini