Baadhi
ya wananchi mkoani Katavi licha ya kuipongeza serikali ya awamu ya
tano, kwa mpango wake wa kuijenga barabara ya Mpanda Koga hadi Tabora
kwa kiwango cha Lami, lakini wameiomba serikali iharakishe kulikarabati
daraja la mto Koga lililoathiriwa na mvua za masika, kwani kufungwa kwa
barabara hiyo kwa zaidi ya miezi mitatu sasa kumewaathiri mno kiuchumi.
Wakiongea na ITV baadhi ya wananchi hao hasa wa kutoka wilaya ya
Mlele mkoani Katavi, wamesema kufungwa kwa barabara hiyo kufuatia ubovu
wa daraja la mto Koga, kumeleta athari kubwa katika masuala ya usafiri
na usafirishaji wa mazao na bidhaa mbalimbali, kwani hivi sasa ukitaka
kwenda Tabora hadi Mwanza na maeneo mengine, inakupasa kuzungukia Uvinza
mkoani Kigoma na kuongeza gharama.
Wakiongelea juu ya mradi huo mkubwa wa ujenzi wa barabara hiyo ya
Lami yenye urefu wa zaidi ya kilomita 342, baadhi ya viongozi wa wilaya
za Mlele na ile ya Sikonge mkoani Tabora itakapopita barabara hiyo,
wamesema ni ufumbuzi wa usafirishaji wa mazao yao ya Asali, Nta, Tumbaku
na hata Ufuta, na hivyo kukuza uchumi wa wananchi wa wilaya hizo.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini