Zaidi
ya wakazi elfu sita wa wilaya mpya ya Malinyi mkoani Morogoro wanakosa
huduma muhimu za kijamii ikiwemo elimu, afya na mahitaji mengine ya
kawaida ikiwemo vyakula na bidhaa, baada ya kukatika kwa mawasiliano ya
barabara kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha na ujenzi uliosimama wa
makalavati katika maeneo mbalimbali.
ITV imetembelea maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo na kushuhudia hali
hiyo, ikiwemo katika eneo la Butu kijiji cha Tanga, ambapo mawasiliano
ya upande mmoja wa kwenda vijiji vilivyopo tarafa ya Ngoheranga
yamekatika baada ya mkandarasi aliyekuwa akijenga kipande cha barabara
ya Lupiro-Malinyi hadi Kilosa kwa mpepo inayosimamiwa na Tanroads
kuitelekeza barabara hiyo kutokana na mvua, hali iliyosababisha maji
kuzingira eneo hilo na wakazi kushindwa kuvuka kutoka upande mmoja
kwenda mwingine, isipokuwa kwa kutumia matrekta au pikipiki ambazo pia
hupita kwa tabu eneo hilo, huku wajawazito,wagonjwa na wafanyabiashara
wakiathiriwa zaidi na hali hiyo.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Malinyi Said
Msomoka na mbunge wa jimbo la Malinyi Dk Haji Mponda pamoja na kukiri
changamoto iliyopo ya barabara katika maeneo mengi ya wilaya hiyo,
sambambà na mazao kuathiriwa na maji kutokana na kufurika kwa mto Furua
unaohitaji kujengewa tuta, wamesema suluhsho la kudumu la changamoto
hizo ni kuanzishwa kwa mkoa mpya utakaozijumuisha wilaya za Ulanga,
Malinyi na Kilombero, pamoja na ulipaji haraka wakandarasi na malipo,
masharti na vigezo vya tenda kuzingatia hali halisi ya maeneo badala ya
unafuu wa gharama unaofanya wakandarasi wasio na uwezo kukubali tenda na
kushindwa kuzimudu.
Mkuu wa wilaya ya Ulanga anayesimamia pia wilaya mpya ya Malinyi
Christina Mndeme amekiri serikali kutambua tatizo hilo na tayari
wakandarasi wamerudi katika baadhi ya maeneo kuendelea na kazi hivyo
kuwasihi wananchi kuwa na subira kwa kipindi hiki.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini