MKURUGENZI
wa Taasisi ya Tanzania na Maendeleo, Khamis Mgeja, amesema Rais mstaafu
wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, anapaswa kuwa mtuhumiwa wa kwanza
kupandishwa kizimbani katika mahakama ya mafisadi inayotarajiwa
kuanzishwa Julai mwaka huu.
Amesema kiongozi huyo ndiye alihusika na kuisababishia hasara Serikali ikiwamo kuota mizizi ya ufisadi serikalini.
Mgeja
amesema pia kuwa Rais Dk. John Magufuli, anapaswa kuendeleza mchakato
wa Katiba Mpya au kufanya marekebisho ya haraka katika baadhi ya sheria
zinazowalinda viongozi kama njia ya kuondoa mfumo unaokumbatia wahalifu.
Hayo aliyasema Dar es Salaam jana alipozungumza na waandishi wa habari.
Alisema Rais Magufuli akiamua kutenda haki katika kuwawajibisha mafisadi na wahujumu uchumi anapaswa kuanza na Rais Mkapa.
“Juzi,
Mkapa tumemsikia kwenye mdahalo anaomba radhi, angekuwa muungwana
angeenda mahakamani kwa makosa aliyowatendea watanzania, tunamuomba rais
Magufuli aanze kumshughulikia Mkapa kupitia mahakama ya mafisadi na
wahujumu uchumi aimbie dunia makosa aliyoyafanya.
“Mkapa ni jipu ila limekaa pabaya ikiwezekana rais asaidiwe,” alisema Mgeja.
Mgeja
alikuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Mkoa wa Shinyanga kabla
ya kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakati wa
Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.
Alisema
Rais mstaafu Mkapa ndiyo chanzo cha nchi kuwa maskini kwa kuwa aliuza
rasilimali kwa bei ya kutupwa na kuruhusu ubinafsishwaji holela
nchini.
“Utetezi
anaoendelea kuutoa kwa wananchi majukwaani baada ya kutoka madarakani
haujitoshelezi kwa kuwa makosa aliyoyafanya ni mazito, angekuwa
muungwana angeenda mahakamani kutuomba radhi,” alisema Mgeja.
Alisema
taasisi hiyo haimani kama Mkapa alifanya mambo hayo kwa bahati mbaya
kwa kuwa alikuwa akitoa uamuzi kupitia Ikulu ambayo ni taasisi yenye
wataalamu ambao wangeweza kumshauri vizuri au hata kumzuia.
“NBC
kaiuza kwa Sh bilioni 16 wakati ilikuwa na mali ya zaidi ya Sh bilioni
100 … wakati anatoa uamuzi huo alikuwa mzima au alikuwa amejitwanga
(kulewa) kwa sababu ni mwanachama mzuri wa hiyo kitu,” alisema Mgeja.
Akizungumzia
uamuzi wa aliyekuwa mmoja wa wanachama wa Chadema, Goodluck ole Medeye
kuhamia UDP, alisema mpaka sasa anaona Chadema ndiyo chama pekee cha
upinzani ambacho kina nguvu ya kuondoa CCM katika dola.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini