Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), amewasilisha mahakamani hati ya kupinga dhamana kwa washtakiwa wa kesi ya kusafirisha tumbili 61 kwenda nchini Armenia.
Hata hivyo, jopo la mawakili watano wa utetezi
wakiongozwa na wakili maarufu kutoka jijini Dar es Salaam, Majura
Magafu, walipinga hati hiyo wakidai haijawasilishwa kihalali mahakamani.
Hati hiyo iliwasilishwa Mahakama Kuu Moshi jana na mawakili wa
Serikali, Wancho Simon na Salim Msemo, muda mfupi kabla ya kuanza
kusikilizwa kwa maombi ya dhamana ya washtakiwa hao.
Akiwasilisha
pingamizi la hati hiyo mbele ya Jaji Mfawidhi, Aishiel Sumari, Wakili
Magafu alisema DPP alipaswa kuwasilisha hati tatu tofauti kwa kila
maombi badala ya kuwasilisha hati moja.
“Hati hii iliwasilishwa
kabla ya amri ya Mahakama yako ya kuyaunganisha maombi ya dhamana ya
washtakiwa, kwa hiyo DPP alipaswa kuwasilisha hati kulingana na kila
maombi,” alidai Magafu.
Alisema maombi yao ya dhamana
yamesajiliwa kwa namba 3/2016, 4/2016 na 5/2016, DPP alitakiwa
kuwasilisha hati tatu tofauti kwa maana ya hati moja kwa kila maombi
yaliyoko kortini.
“Hoja yetu hapa ni je hati hii ya DPP iko
sahihi mbele ya Mahakama yako? Ombi letu ni uitupilie mbali na ombi letu
la dhamana lisikilizwe,” aliomba Magafu.
Hata hivyo, wakili
huyo alisema kama Mahakama itaona hati hiyo imewasilishwa kihalali, basi
iwaruhusu kuzungumzia uhalali wa hati yenyewe kisheria na madhara yake.
Akijibu hoja hiyo, Wakili Simon alisema wakili mwenzake
(Magafu) anaipotosha Mahakama na hakunukuu sheria yoyote inayoipa nguvu
hoja yake ya kupinga hati hiyo ya DPP.
Wakili huyo alifafanua,
hata hati za kuitwa shaurini walizotumiwa hazikuwa tofauti kulingana na
namba za maombi, bali walitumiwa hati moja ikitaja maombi yote sehemu
moja.
Akitoa uamuzi mdogo kuhusu mabishano hayo, Jaji Sumari
alisema amepitia kwa umakini hati ya DPP na kujiridhisha kuwa iko sahihi
mbele ya Mahakama.
Hata hivyo, Jaji Sumari alisema hoja ya hati
hiyo imewasilishwa kabla ya wakati na kuutaka upande wa mashtaka
kuwasilisha kwanza kiapo kinzani leo.
Alisema kama mawakili wa
utetezi watakuwa na majibu ya ziada kutokana na kiapo hicho kinzani,
wawasilishe majibu kesho na majibizano yasikilizwe Aprili 14, mwaka huu.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini