WATU 79 wamekamatwa na Idara ya Uhamiaji nchini kwa kosa la kuishi nchini bila vibali na kufanya kazi wasizo na taaluma nazo.
Naibu Kamishna wa Uhamiaji Dar es Salaam, John Msumule jana alisema watuhumiwa hao wanatoka katika nchi 15.
Nchi
hizo na idadi ya wahamiaji haramu ni Nigeria (4), China (20), Ethiopia
(23), Korea (9), Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC (6), Somalia
(3),Uganda (2), Madagascar (5), Burundi (2), Ivory Coast (1), Lebanon
(1), India (1), Zimbabwe (1) na Ghana (1).
Alisema
katika ‘kamata kamata’ hiyo pia wamefanikiwa kukamata Watanzania
watatu, ambao wamekuwa wakijishughulisha na kukusanya, kuwahifadhi na
kuwasafirisha wasichana kuwapeleka nchi za mbali, kwa ajili ya kufanya
kazi mbalimbali.
“Tumewakamata
wasichana sita ambao walikuwa wamekusanywa na watanzania hao ili
kusafirishwa na tutawachukulia hatua za kisheria ili kutoa fundisho kwa
wengine wenye nia ya kufanya mtindo kama huu,” alisema Msumule.
Aliongeza
kuwa idara hiyo imewarudisha nchini mwao wahamiaji 23 raia wa Ethiopia
na watuhumiwa nane wa nchi mbalimbali,wamefikishwa mahakamani. Alisema
shughuli ya kuwarejesha raia wengine katika nchi zao zinaendelea.
Msumule
aliwataka wamiliki wa nyumba za kulala wageni na nyumba za kupanga,
wahakikishe wanatambua wateja wao ni raia wa wapi na anafanya kazi gani,
kabla ya kufanya naye mkataba wa aina yoyote.
Aliwataka
pia watanzania wanaooa na kuolewa, wahakikishe wanafahamiana na mtu
huyo na kumchunguza kujua anakotoka na yupo nchini kwa kazi gani, la
sivyo mtu akibainika anaishi na mhamiaji, anaweza kujiingiza katika
matatizo.
“Sisi
hatutajali, tutamkamata kwa kosa la kumhifadhi kwa hiyo lazima wajenge
dhana ya kuwachunguza watu hao, hata wasichana wa kazi za ndani, lazima
umjue vizuri na sio unamchukua tu bila kujua historia yake ,” alisema.
Msumule
aliwataka raia wengine ambao hawana vibali vya kuishi nchini, waondoke
wenyewe na wasisubiri hadi sheria ichukue mkondo wake.
“Wapo wengi, tunachoomba waondoke wenyewe bila kushurutishwa, wengine wanafanya kazi ambazo hata watanzania wanaweza kuzifanya, wakubali na waondoke,” aliagiza.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini