SERIKALI
imesema haitosita kuwafungulia mashtaka na kuwapeleka mahakamani
ifikapo Machi 30, mwaka huu, wazazi ama walezi wote watakaoshindwa
kupeleka watoto wao shuleni ili kupata elimu ya msingi na sekondari.
Aidha,
imepiga marufuku kwa jamii kutumia jina la ‘watoto wa majumbani’,
badala yake waitwe wasaidizi hao ‘wasichana wa kazi’ au ‘vijana wa
kazi’. Hayo yalisemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, Dar es Salaam jana.
Alisema hayo ili kuhamasisha wazazi na walezi juu ya watoto kujiunga na shule za msingi na sekondari kwa mwaka huu 2016.
Kuhusu
kuwafungulia wazazi mashtaka, alisema serikali inaamini kuwa ikiwa
inataka kujenga taifa lililoelimika ni lazima kuwekeza kwenye elimu,
hivyo ni wajibu wa kila anayehusika kuhakikisha anatimiza wajibu wake.
“Elimu
ndio njia bora ya kuwajengea watoto wetu msingi imara wa maisha
yao…serikali haitosita kuchukua hatua za kisheria kwa wazazi au walezi
ambao watazembea, kumficha, kumtorosha au kuzuia mtoto kuanza masomo ya
shule za msingi na sekondari,” alisema Ummy.
Alisema
serikali kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, itawafungulia
mashtaka na kuwapeleka mahakamani wazazi na walezi wote watakaoshindwa
kutimiza wajibu wao wa kuwapeleka watoto shule, kwani hata Sheria ya
Mtoto Namba 2 ya mwaka 2009 Kifungu cha 8, inaelekeza kuwa ni wajibu wa
mzazi kuhakikisha mtoto anapata elimu.
Waziri
Ummy alisema Kifungu cha 14 kinatamka kuwa ni kosa la jinai, kushindwa
kutimiza wajibu huo na adhabu yake ni faini isiyozidi Sh milioni 5 na
kifungo kisichozidi miezi 6; au vyote kwa pamoja.
Alisema
pia wazazi na walezi, wahakikishe kuwa watoto wanaoendelea na masomo ya
shule ya msingi na sekondari, wanahudhuria masomo yao kwa ufanisi, kwa
kuwa serikali haitarajii kuendelea kuona utoro wa watoto shuleni
kutokana na sababu zinazoweza kuepukika.
Kuhusu
kuwepo kwa mwitikio mkubwa wa watoto wanaoanza masomo, alisisitiza kuwa
wazazi, walezi na jamii kuhakikisha kila mtoto mwenye umri wa kuanza
elimu ya msingi yaani darasa la kwanza na elimu ya awali, kujiunga na
shule kwa muda uliopangwa na kuhudhuria masomo ipasavyo.
Kuhusu
kuwepo kwa michango mbalimbali katika baadhi ya shule wakati huu wa
maandalizi ya shule, alisema serikali imeshatoa mwongozo stahiki.
Waziri
huyo alisisitiza kwamba sio ada peke yake iliyofutwa, bali hata
michango yote na tayari serikali imekwishatoa fedha za kugharimia elimu
bure na zimekwishapelekwa katika shule zote nchini.
Kwa
ujumla, walimu wakuu hawatakiwi kutoza mchango wa aina yoyote, kama
vile ya ulinzi, maji, umeme, uzio, fagio, jembe, ndoo na mingineyo,
kwani fedha za kugharimia elimu ya bure zitatumika pia kwenye masuala
hayo yote
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini