Wananchi zaidi ya 100, wakiwemo waliobomolewa maeneo ya mabondeni jijini Dar es Salaam, wamevamia shamba la Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye lenye ukubwa wa heka 33, lililopo Mji Mpya eneo la Mabwepande na kujikatia viwanja.
Sumaye
ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa serikali ya awamu ya tano kati ya mwaka
1995 hadi 2005, amekiri wananchi kuvamia shamba hilo lakini alisema hana
wasiwasi kwasababu ana hati za umiliki.
Aidha alisema atafuata mkondo wa sheria kuhakikisha wavamizi hao wanaondoka kwenye shamba lake.
Juzi
mwandishi alishuhudia wananchi kadhaa wakiendelea kujenga nyumba za
miti na wengine za matofali baada ya kujigawia kila mmoja eneo lake
kwenye shamba hilo.
Musa
Juma, aliyekutwa kwenye shamba hilo akijenga nyumba, alisema yeye ni
miongoni mwa waathirika wa bomoa bomoa iliyofanyika Kinondoni Mkwajuni
na kwamba amefika hapo baada ya mwenzao aliyemtaja kwa jina moja la Ema
kuwaeleza kuwa kuna pori la Sumaye alilolitelekeza.
“Mwenzetu
Ema alikuja kule bondeni tulikobomolewa na kutupa habari hiyo hivyo
watu kama 100 tukaamua kuja na tukawakuta wengine tuliliona shamba hili
likiwa ni pori kubwa ndipo tukaanza kujigawia vipande vipande,” alisema.
“Tumefanya
kazi kubwa ya kulifyeka mpaka unaliona lipo katika hali hii, kazi
haikuwa ndogo, tumekutana na nyoka wakubwa, ukishuka kule bondeni kwenye
kingo za shamba utajionea mwenyewe jinsi pori hili lilivyokuwa.”
Juma
alisema walivamia shamba hilo mwezi Oktoba mwaka jana, na wengine
walikuja baadaye baada ya kupata taarifa kuwa kuna shamba la bure ambalo
limetelekezwa akiongeza kuwa wako pia watumishi wa serikali waliovamia
shamba hilo.
“Aliwahi
kuja mwanamke mmoja ambaye hatumfahamu akidai kuwa yeye ni mke wa
kiongozi huyo na kutueleza kuwa tunapaswa kuondoka eneo hili eti ni mali
yao lakini juzi kaja mwenyewe Sumaye; akatusalimia na kuondoka bila
kusema lolote,” alisema.
“Mwamamke
yule alikuja na watu wengine akiwemo mtu ambaye alikuwa akipiga picha
na baadaye aliondoka hadi Alhamisi ya wiki hii walivyokuja wote na
Sumaye mwenyewe ingawa hakusema lolote mpaka anaondoka hapa.
“Sumaye
alikuja kwa sababu Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda, aliitisha
mkutano na wananchi wa hapa, lakini tukiwa tumekusanyika tukimsubiria
Makonda ghafla alifika Sumaye, ambaye hakushuka kwenye gari lake,
alitusalimia kwa kutunyooshea mikono na kuondoka kwasababu Makonda hakuja siku hiyo.”
Alipoulizwa
sababu za kuvamia shamba hilo, alisema walimsikia Rais John Magufuli
kwenye kampeni akisema kuwa mashamba yote ambayo hayajaendelezwa
yarudishwe serikalini na wapewe watu wenye uwezo wa kuyaendeleza.
Juma alisema wamejigawia shamba hilo na sasa wanasubiri serikali ije kuidhinisha kwa kuwamilikisha wao.
“Mtu
anahodhi shamba kubwa kama hili halafu halijapimwa, tumetafuta alama za
mipaka hakuna, wakati mashamba yote yaliyolizunguka shamba hili
yamepimwa,” alisema.
Sumaye
alisema anamiliki shamba hilo kihalali na ana hati zote na kwamba upo
utaratibu wa kuchukua mashamba yaliyotelekezwa lakini sio huo
walioutumia wananchi hao.
“Shamba
hatujalitelekeza kama wanavyodai hao wananchi, tuna hati na ni letu
kihalali, wanasema halina alama za mipaka je, waulize hati nilipataje?
Shamba lina alama labda kama wamezing’oa kwa sababu ya jeuri.”
Sumaye
alisema juhudi za kuhakikisha shamba hilo linarudishwa mikononi mwake
zimeanza kufanyika na mamlaka husika na kusisitiza kuwa hatatumia nguvu
kuwaondoa zaidi ya kufuata sheria.
Kuhusu
kuonekana eneo hilo siku ya Alhamisi, Sumaye alisema alienda huko kwa
sababu Makonda aliitisha mkutano na wananchi ili kutafuta suluhu ya
mgogoro huo lakini hakufika baada ya kupata udhuru.
Mwenyekiti
wa Serikali ya Mtaa, Jastine Chiganga, alisema alipigiwa simu na
Makonda akimweleza kuhusu mkutano huo lakini hakuweka bayana sababu za
kuuitisha, ingawa aliuahirisha baada ya kupata dharura.
Makonda
alilipoulizwa kuhusu lengo la mkutano aliouitisha na baadaye
kuuairisha, alisema lilitokana na ofisi yake kupokea malalamiko ya
uvamizi wa mashamba unaofanywa na wananchi eneo hilo.
Alisema
baada ya kupokea malalamiko hayo aliomba kukutana na viongozi wa mitaa
husika, wananchi, watu wa ardhi na wamiliki wa mashamba hayo ili kujua
ukweli kuhusu mgogoro huo.
“Hilo
shamba linalodaiwa kuwa ni la Sumaye, sijawahi kupokea malalamiko
kutoka kwake dhidi ya uvamizi huo ila niliwahi kupigiwa simu na mmoja wa
Makamanda wa Polisi Mkoa ambaye alinieleza kuhusu uvamizi huo,” alisema.
Aidha,
Makonda alisema mbali ya shamba hilo la Sumaye yapo mengine likiwemo la
Gavana wa zamani wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), marehemu Daudi Ballali
ambalo nalo limevamiwa.
Alisema mkutano wake aliouitisha ulilenga kwenda kupata taarifa kamili ili hatua ziweze kuchukuliwa.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini