TAARIFA KWA VYOMBO
VYA HABARI
WAZIRI MKUU
AFURAHISHWA NA HALI YA CHAKULA MKOANI RUVUMA
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amefurahishwa na hali ya chakula mkoani Ruvuma, ikiwa kati ya mikoa
inayotegemewa kwa uzalishaji wa chakula kwa wingi nchini.
Akizungumza na viongozi wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali jana jioni (Jumapili, Januari 3, 2016)
katika ukumbi uliopo Ikulu ndogo Songea, Waziri Mkuu ameutaka
uongozi wa mkoa kuhakikisha kuna upatikanaji wa masoko kwa mazao mbalimbali
pamoja na kuendelea kutoa msukumo kwa wananchi.
Pia, ameupongeza uongozi wa
mkoa huo kwa kutoa msukumo kwa wananchi na kufanyakazi, na kusema ni jambo
linalosaidia kupanda kwa pato la mtu mmoja mmoja, hata hivyo hakusita
kuwashukuru kwa mapokezi makubwa aliyopata.
“Nawapongeza sana wana
Ruvuma kwa kuongeza pato la ndani kutoka shilingi 654,227, hadi kufikia
shilingi 1,800,000 kwa kipindi cha mika 4 tuendelee kujiweka vizuri kwa
kuongeza pato la mtu mmoja mmoja” alisema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu Majaliwa pia amesisitiza
kilimo cha umwagiliaji katika maeneo yote yenye mabonde ili wakulima waweze
kuvuna bila kutegemea sana kipindi cha masika. Amesema ni lazima kuimarisha
huduma muhimu na kusisitiza matumizi mazuri ya fedha zinazopatikana
katika mazao hayo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Thabit Mwambungu
amesema zaidi ya asilimia 90 ya wananchi wa Ruvuma hutegemea kilimo cha
mazao mbalimbali ya chakula na biashara yakiwemo mahindi, mpunga
ambao unalimwa sehemu za Tunduru na Songea vijijini, korosho ambazo
zinalimwa sehemu za Tunduru, Namtumbo, Nyasa, Mbinga na Songea vijijini na
tumbaku maeneo ya Namtumbo,Mbinga na Songea vijijini.
Alisema, Ruvuma imekua
ikizalisha chakula kwa kiwango cha utoshelezi na ziada kwa kipindi cha mwaka
2012 - 2013, 2013 - 2014 hali hiyo imeendelea kuwa nzuri hadi kipindi cha mwaka
2015 - 2016. Mahitaji yakiwa ni tani 469,172 na ziada ikiwa tani 1,950,111,
ametaja baadhi ya sababu za ongezeko hilo la tani ni pamoja na matumizi
ya dhana bora za kilimo, matumizi ya pembejeo za kisasa na urahisi wa
upatikanaji wa pembejeo, aliongeza Mkuu wa Mkoa.
Waziri Mkuu Majaliwa ambaye
jana (Jumapili, Januari 3, 2016) ameanza ziara ya kikazi ya siku nne mkoani
Ruvuma, leo siku ya jumatatu atakuwa na shughuli za
kufungua tawi la Benki ya Posta mjini Songea, kukagua maghala ya
Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya chakula (NFRA) kanda ya Songea na
kukagua Makao Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Songea.
Kupitia
ziara hii Serikali ina lengo la kuona hali halisi ya utendaji wa shughuli za
maendeleo kutoka kwa watendaji mbalimbali, kuwatia moyo na kuweka msisitizo
katika maeneo yaliyopewa kipaumbele hasa katika sekta ya Afya.
IMETOLEWA
NA:
OFISI YA
WAZIRI MKUU,2 MTAA
WA MAGOGONI,
S. L. P
3021,11410
-DAR ES SALAAM
JUMATATU,
JANUARI 4, 2016.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini