MAKAMU
wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amesema juhudi
za kuutafutia ufumbuzi mkwamo wa kisiasa Zanzibar zinaendelea, na
kuwataka wananchi waendelee kuwa watulivu.
Amesema
katika kipindi hiki cha mazungumzo maneno mengi ya kuwavunja moyo
wananchi hasa kutoka vyama vya upinzani yatasemwa, lakini amesema
ufumbuzi wa tatizo hilo utapatikana kwa kuheshimu misingi ya katiba na
sheria za nchi.
Maalim
Seif ametoa kauli hiyo huko Hoteli ya Bwawani mjini Zanzibar katika
salamu zake za kuwakaribisha waumini wa dini ya Kiislamu waliohudhuria
Maulid ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (SAW).
Amesema
katika kuutafutia ufumbuzi mzozo huo, atahakikisha kuwa maamuzi ya
wananchi waliyoyafanya tarehe Oktoba 25, 2015 kwa kuchagua viongozi
wanaowataka yanaheshimiwa.
Ameeleza
kuwa amefanya Maulid hayo ya kila mwaka huku nchi ikigubikwa na mkwamo
wa kisiasa, na kusisitiza kuwa ufumbuzi wake utapatikana kwa kuzingatia
matakwa ya kikatiba na sheria.
Maalim
Seif ambaye ni mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Wananchi
(CUF), ametoa kauli hiyo siku moja tu baada ya Rais wa Zanzibar Dk Ali
Mohamed Shein kutamka hadharani kuwa yeye ni Rais halali wa Zanzibar kwa
mujibu wa Katiba, na kuwataka wasioridhika waende mahakamani.
Aliwashukuru
wananchi kwa kujitokeza kwa wingi hatika hafla hiyo ya Maulid, na
kuwataka waendeleze umoja na mshikamano wao, sambamba na kudumisha amani
na utulivu.
“Najua kuwa yatasemwa mengi katika kipindi hiki, lakini narejea wito wangu kwa wananchi kuwa msichokozeke”, alisisitiza Maalim Seif.
Hafla
hiyo ya Maulid iliyoishirikisha Madrasat Nuur Islamiyya ya Ukutani
Zanzibar, imehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Rais mstaafu wa
Zanzibar Dk Amani Abeid Karume, aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF Taifa
Profesa Ibrahim Lipumba pamoja na Mzee Hassan Nassor Moyo.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini