Wabunge
wote wa Chama cha Wananchi (CUF) wametangaza rasmi kutomtambua
aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.
Wamemtaka
Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi kutomkumbatia
mwanasiasa huyo aliyebobea katika uchumi, ikielezwa kwa sasa hana sifa
za kuwa mwenyekiti wa chama hicho, labda aanze upya mchakato.
Wameeleza
msimamo huo jana mjini Dodoma na Mbunge wa Viti Maalumu, Riziki Mngwali
ambaye pia ni Kiongozi wa Wabunge wa CUF katika mkutano baina ya
waandishi wa habari za Bunge na wabunge wa CUF isipokuwa Mbunge wa Jimbo
la Kaliua, Magdalena Sakaya aliyesimamishwa uanachama, ingawa
anaendelea kutimiza majukumu yake bungeni.
Mngwali
alisema Profesa Lipumba amekuwa akijaribu kukiyumbisha chama na hivi
karibuni kudai amekaririwa akisema anasubiri barua ya Msajili wa Vyama
vya Siasa ya kuthibitishiwa kuendelea na uenyekiti wake.
“Wakati
anajiuzulu uenyekiti Agosti 5, mwaka jana aliutangazia umma na kudai
anakwenda Rwanda kwa kazi aliyodai ya utafiti ili aje kuisaidia
serikali, lakini inashangaza sasa anataka kujirejeshea uenyekiti. Hilo
hatukubali kwa kuwa chama kina taratibu zake,” alisema.
Aliongeza
kuwa, alikiacha chama katika wakati mgumu kuelekea Uchaguzi Mkuu,
lakini kikaimarika zaidi kwa kupata wabunge 43, madiwani 287, kuongoza
manispaa mbili na halmashauri za wilaya tatu, hivyo wanashangazwa kuona
akitaka kurejea, tena kwa kutumia nguvu.
“Tunataka ifahamike kwa dhati kuwa, sisi wabunge, hatumtambui tena Profesa Lipumba kama Mwenyekiti wa CUF,” alisema Mngwali na kumtaka Msajili kutomuidhinisha Lipumba, kitendo alichodai kitachochea mgogoro ndani ya chama.
Aliongeza
kuwa badala ya kutumia mabavu kutaka kurejea madarakani, ni vyema
akabaki na heshima yake, kwani amekitendea mambo mengi chama hicho na
kwamba wanamheshimu, hivyo afuate taratibu za kichama kutaka kuwania
tena uenyekiti.
Mngwali
alisema wamekubaliana na uamuzi wa Baraza Kuu la Uongozi wa CUF wa
kuwasimamisha uanachama Lipumba na wenzake tangu Agosti 28, 2016
kutokana na kile kinachodaiwa kukiuka Katiba ya chama hicho.
Miongoni
mwa tuhuma zao ni kusababisha vurugu wakati wa Mkutano Mkuu Maalumu wa
Uchaguzi Agosti 21, mwaka huu jijini Dar es Salaam uliokuwa unalenga
kumthibitisha Juma Duni Haji kuwa Mwenyekiti mpya.
Hata
hivyo, kutokana na vurugu zilizoibuka, mkutano huo ulivunjika. Mbali ya
Lipumba na Sakaya, wengine waliositishiwa uanachama ni Abdul Kambaya
ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, Ashura
Mustapha, Omar Mhina, Thomas Malima, Kapasha M. Kapasha, Mohamed Habib
Mnyaa, Haroub Shamis na Mussa Haji Kombo.
Ashura
ni mjumbe wa Baraza Kuu na aliwahi kuwa Naibu Mkurugenzi wa Habari na
Mawasiliano ya Umma CUF wakati Mnyaa na Kombo, walikuwa wabunge kipindi
cha 2010/2015, Mnyaa akiwakilisha Jimbo la Mkanyageni na Kombo Jimbo la
Chake Chake, kisiwani Pemba.
Kutokana
na kusimamishwa kwa viongozi hao, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Nassor
Ahmed Mazrui alimtangaza Julius Mtatiro aliyewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu
Bara kuwa kiongozi wa Kamati ya Uongozi wa muda inayowajumuisha pia
wabunge Katani Ahmed Katani na Savelina Mwijage ambao ni wajumbe wa
Baraza Kuu la Uongozi la Taifa.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini