Na Ismail Ngayonga - Maelezo.
SERIKALI
inakusudia kuwapeleka katika kambi za mafunzo ya Jeshi la Kuujenga
Taifa (JKT) watoto wa mitaani wenye umri wa zaidi ya miaka 18 ili
wajifunze stadi za kazi na shughuli za uzalishaji mali.
Hayo
yamesemwa jana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu wakati wa mahojiano maalum katika kipindi cha
Tunatekeleza kinachoandaliwa na Idara ya Habari (MAELEZO) na
Televisheni ya Taifa (TBC1).
Waziri
Ummy alisema hatua hiyo inalenga kuliwezesha kundi hilo la vijana
kujihusisha na shughuli za uzalishaji mali badala ya kuzurura hovyo
mitaani sambamba na kujihusisha na tabia na vitendo vinavyokiuka
maadili katika jamii.
Alisema
tayari watendaji wa Wizara yake kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Waziri Mkuu
tayari wamekutana kujadiliana kuhusu suala hilo ili kuangalia namna bora
zaidi ya kusadia kundi hilo.
Alifafanua
kuwa vituo vingi vya kulelea watoto hao vimekuwa na watoto waliozidi
umri wa miaka 18, ambapo kwa mujibu wa sheria hawatakiwi kuwa katika
vituo hivyo na kuongeza kuwa ofisi yake itahakikisha zoezi la
kuwapeleka katika mafunzo hayo linatekelezeka.
Katika
hatua nyingine Waziri Ummy alipiga marufuku tabia za baadhi ya watu,
asasi na vikundi kuanzisha vituo vya kulea watoto yatima pasipo kuwa na
usajili kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Kwa
mujibu wa Waziri Ummy alisema tayari ofisi yake imetoa maelekezo kwa
Kamishina wa Ustawi wa jamii kufanya tathimini na utafiti wa kina kuhusu
vituo vya kulea watoto yatima, ambapo iwapo kutabainika vituo
vitakavyokosa sifa hatua za kisheria zitachuliwa kwa wahusika.
Kuhusu
chanjo, Waziri Ummy alisema Serikali itaanza kutoa chanjo ya saratani
ya shingo ya kizazi kwa watoto wenye umri wa miaka 9-13 ili kukabiliana
na changamoto ya maradhi hayo nchini.
Waziri
Ummy aliwataka wazazi kutoa ushirikiano pindi zoezi hilo litakapoanza
kwa kuwa halitakuwa na madhara ya kiafya kwa watoto wao.
Aidha,
alisema Serikali imekuwa ikipoteza kiasi kikubwa cha fedha kila mwaka
kwa ajili ya matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo saratani ya
shingo ya kizazi kwa akina mama ambayo inaambukizwa na virusi
vinavyojulikana kwa jina la Human Papiloma Virus (HPV).
“Tumeamua
kuteua kundi la watoto wa lika huo kwani wengi wao katika umri huo
wanakuwa bado hawajaanza kujihusisha na vitendo vya mapenzi” alisema Waziri Ummy.
Alisema
katika bajeti ya mwaka 2016/17 Serikali imepanga kuipatia taasisi ya
saratani ya ocean road kiasi cha Tsh. Bilioni 3 kwa ajili ya ununuzi wa
madawa, ikilinganishwa na kiasi cha Tsh. Milioni 600 zilizokuwa
zimetengwa katika bajeti ya mwaka 2015/16.
Akizungumzia
changamoto iliyojitokeza hivi karibuni ya ukosefu wa chanjo katika
vituo vya huduma ya hivi nchini, Waziri Ummy alisema suala hilo litakuwa
historia hivi karibuni kwani tayari Serikali imeagiza kutoka nje ya
nchi baadhi ya chanjo hizo.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini