Serikali imewahakikishia Watanzania kuwa inaendelea na mikakati ya makusudi katika kudhibiti ongezeko la deni la taifa.
Hayo
yamesemwa na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Ashatu Kijaji
alipokuwa akijibu swali la Saed Kubenea Mbunge wa Ubungo lililouulizwa
kwa niaba yake na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Hai
Freeman Mbowe lililohusu deni la taifa.
Naibu
Waziri huyo aliitaja mikakati inayosaidia kupunguza deni la taifa
ambayo ni pamoja na kuongeza ukusanyaji wa mapato, kupunguza matumizi
yasiyo ya lazima, kuendelea kutafuta misaada na mikopo nafuu na kukopa
mikopo michache ya kibiashara ya miradi yenye kuchochea kwa haraka
ukuaji wa pato la taifa.
Mikakati
mingine ni kudhibiti ulimbikizaji wa madai ya kimkataba kwa wakandarasi
na watoa huduma na kudhibiti madeni yatokanayo na dhamana za Serikali
kwenye mashirika ya umma kwa kufanya ufuatiliaji wa karibu wa mikataba
inayoweza kusababisha mzigo wa madeni kwa Serikali.
Naibu
Waziri Dkt. Ashatu alisema hadi kufikia Juni 2016 deni la taifa
lilikuwa dola za kimarekani bilioni 23.2 ikilinganishwa na dola bilioni
19.69 kwa mwezi Juni 2015 ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 18.
Dkt.
Ashatu alifafanua kuwa kati ya kiasi hicho, deni la Serikali ni dola za
Kimarekani bilioni 20.5 na deni la sekta binafsi ni dola za
Kimarekani bilioni 2.7 na kuongeza kuwa deni la Serikali linatokana na
mikopo ya ndani na nje kwa ajili ya kugharimia miradi ya maendeleo.
Baadhi
ya miradi ya maendeleo iliyoainishwa ambayo imetumia fedha za maendeleo
ni pamoja na ujenzi wa barabara na madaraja, mradi ya kimakakati wa
kuboresha majiji, ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kv 400 kutoka
Iringa hadi Shinyanga na mabasi yaendayo haraka.
Miradi
mingine ni ujenzi wa bomba la gesi na mitambo ya kusafisha gesi,
upanuzi wa uwanja wa ndege wa Dar es salaam na mradi wa maji wa Ruvu Juu
na Ruvu Chini.
Aidha,
Dkt. Ashatu amesema kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2010/2011,
Serikali ilipokea mikopo yenye masharti nafuu na ya biashara kiasi cha
sh trilioni 1.3 na mwaka 2014/2015 Serikali ilipokea mikopo ya kiasi cha
Sh. trilioni 2.3 mikopo ambayo haikufikia trilioni 15 kwa mwaka 2011 na
trilioni 9 kabla ya mwaka 2015.
Kwa
upande wake Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi alipokuwa akichangia hoja
hiyo amewatoa hofu Watanzania na kusema kuwa haitatokea hata siku moja
wagongewe milango kwa kudaiwa deni la taifa na kuongeza kuwa deni la
taifa linapimwa kutokana na ukusanyaji wa mapato hatua ambayo Serikali
inaendelea kuitekeleza kwa vitendo.
Waziri
Mwigulu aliongeza kuwa Serikali haikopi kwa ajili ya miradi ya kawaida
isipokuwa inakopa kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa lengo la
kuwahudumia wananchi.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini