Na. Aron Msigwa – Maelezo
Tume
ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) imeyataka mashirika, wadau na
taasisi zilizo katika mapambano dhidi Ukimwi kuzingatia malengo ya awali
ya kuanzishwa kwa taasisi hizo na kuepuka kujiingiza katika shughuli
za uanaharakati ambazo ni kinyume cha sheria.
Akizungumza
katika kikao chake cha kwanza na wadau mbalimbali walio katika
mapambano dhidi ya Ukimwi leo jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mtendaji
wa TACAIDS Dkt. Leonard Maboko amesema kuwa baadhi ya wadau, mashirika
na taasisi zimekuwa zikifanya shughuli nje ya malengo ya awali ya
kuanzishwa hali inayosababisha mgongano katika jamii.
"Zipo
baadhi ya taasisi zinazofanya shughuli nje ya malengo, tunatambua
Serikali haijakataa jitihada za makundi mbalimbali ya kupambana na
UKIMWI, sisi kama TACAIDS tutaendelea kuungana na Serikali kuhakikisha
kuwa zile taasisi zilizo kwenye mapambano zinasimamia malengo ya
kuanzishwa kwake na si vinginevyo" Amesisitiza Dkt. Maboko.
Amewataka
wadau na mashirika hayo kuendelea kujikita na kuongeza nguvu katika
utoaji wa elimu ,uhamasishaji wa wananchi kupima kwa hiari VVU kwa lengo
la kujua hali zao ili waweze kujikinga na maambukizi mapya ya
ugonjwa huo.
Pia
amewata wadau hao kuangalia namna bora ya kuwafikia, kuwaelimisha na
kuwafuatilia wananchi walio katika makundi maalum kwenye mazingira
hatarishi pia kuongeza shughuli za utafiti zitakazoisaidia nchi kufikia
lengo la maabukizi sifuri.
Amesema
hali ya uelewa wa wananchi juu ugonjwa wa Ukimwi imefikia asilimia 90
kwa kuwa watanzania sasa wanauelewa kuhusu ugonjwa huo na hali zao .
Aidha, wengi wana uelewa iwapo wamepata maambukizi au la kutokana na
kuongezeka kwa kampeni za uhamasishaji na elimu ya kujikinga na
maambukizi.
Kwa
upende wake Mkurugenzi wa Chama cha Uzazi na Malezi Bora Tanzania
(UMATI), Lulu Ng’wanakilala amesema Taasisi zinazosajiliwa kutoa huduma
za kuzuia na kupunguza maambukizi dhidi ya Ukimwi nchini Tanzania na
kuanza kujiingiza kwenye shughuli za uanaharakati zinakwamisha na
kupunguza juhudi za Serikali na wadau wengine wenye mapenzi mema walio
kwenye mapambano dhidi ya Ukimwi.
‘Sisi
kama wadau wa hizi taasisi tunaongea lugha moja, NGOs zinazosajiliwa
kutoa huduma na kuanza kufanya uanaharakati kupitia masuala ya Ukimwi
zinakwenda kinyume cha malengo, sisi tupo kwa lengo moja kuhakikisha
maambukizi yanafikia sifuri kuhakikisha wote wanaotakiwa kupata huduma
wanafikiwa na huduma zetu hasa makundi yanayochangia kwa kiasi kikubwa
maambukizi ya Ukimwi’ Amesisitiza.
Naye
Afisa Mtendaji Mkuu wa Baraza la Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi
Tanzania (NACOFA) Bw. Deogratius Peter, akizungumzia hatua ya baadhi ya
taasisi kuenenda kinyume na malengo ya kuanzishwa kwake amesema
‘Serikali
imeshatoa Sera na miongozo mbalimbali inayosimamia shughuli za utoaji
wa huduma za mapambano dhidhi ya Ukimwi kwa taasisi, makundi na wadau
mbalimbali, Sisi pamoja na Serikali tunakubali na kuheshimu juhudi za
makundi haya katika mapambano dhidi ya Ukimwi, suala la uanaharakati
halikubaliki maadili lazima yazingatiwe katika utoaji wa huduma zetu
tufuate sheria za nchi ile kuepusha migongano isiyo ya lazima’
Amesisitiza.
Ameongeza
kuwa taasisi zote zilizo katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi
lazima zikajikite katifa tafiti pia kuyafuatilia makundi yote yaliyo
katika mazingira hatarishi ambayo yanachangia kwa kiwango kikubwa
kueneza maambukizi ya VVU.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini