TAASISI
ya Maridhiano inatarajia kuwasilisha ujumbe kwa Spika wa Bunge Job
Ndugai kuomba kuyakutanisha makundi mawili yanayosigana bungeni ili
kuleta muafaka wenye tija kwa taifa.
Mwenyekiti wa taasisi hiyo Sheikh
Sadick Godigodi jana alisema kumeguka kwa Bunge kunakosababishwa na Kambi ya
Upinzani kuona inaonewa na maamuzi ya Naibu Spika, Dk. Tulia Akson
kunahitaji viongozi wa dini kuingilia kati na kupata suluhu.
"Tunatarajia
katika Bunge lijalo litakaloanza Septemba kuwasilisha ujumbe kwa Spika
ili tupewe nafasi ya kutatua mgogoro huu kwa maana wabunge wote
wanatakiwa kuwepo bungeni kuwakilisha matatizo ya wananchi," alisema
Sheikh Godigodi.
"Haiwezekani kundi moja likawa nje na jingine likaendelea, tunahitaji maridhiano ya pande zote mbili za muhimili huo.”
Kambi ya Upinzani Bungeni ilisusia vikao vya Bunge la Bajeti kwa zaidi ya siku 70 kupinga kile kilichoita kuburuzwa na
Naibu Spika katika uendeshaji wa chombo hicho cha kutunga sheria.
Kambi hiyo, ilianza kutoka nje Mei 30 baada ya Naibu Sika kukataa hoja ya Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua
Nassari
(Chadema), ya kutaka Bunge likatize shughuli zake na kujadili hoja ya
kufukuzwa kwa wanafunzi zaidi ya 700 wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).
Ingawa
kitendo hicho cha Naibu Spika kiliwaudhi wabunge wa chama tawala (CCM)
na Upinzani, kambi hiyo haikurudi ndani mpaka Bunge lilipoahirishwa na
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katikati ya wiki iliyopita.
Mshauri
wa mambo ya kisheria na kidiplomasia wa taasisi hiyo ya Maridhiano,
Agustino Matefu alisema mbali na kusuluhisha migogoro chochezi ya kidini
kwa kutoa elimu sahihi kwa umma, pia wamejikita katika kusuluhisha
migogoro sugu kati ya wakulima na wafugaji nchini.
“Tumetoa
mchango mkubwa wa kuleta suluhu ya migogoro ya ardhi baina ya wafugaji
na wakulima mkoani Morogoro katika wilaya za Mvomero, Kilombero na
Kilosa (na) ndio maana watanzania wanaona hali ni kama sasa imekuwa
shwari,” alisema Matefu.
Matefu alisema wamepata mualiko rasmi kwa
uongozi wa Mkoa wa Iringa na wanatarajia kwenda huko baada ya uzinduzi
rasmi wa taasisi hiyo utakaofanyika Julai 13 jijini Dar es Salaam.
Katibu
wa taasisi hiyo, Mchungaji Oswald Mlay alisema kuwa uzinduzi na
utambulisho wa taasisi hiyo utaendana na utoaji tuzo ya amani kwa
viongozi na watu mbalimbali waliojitoa kuhamasisha udumishwaji wa amani
nchini.
Wanaotarajiwa kupewa tuzo ni Mama Maria Nyerere kwa niaba
ya Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere ambae atatunukiwa tuzo ya Amani
uasisi wa amani ya taifa.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini