WAKATI Rais Dk. John Magufuli akitarajiwa kumwapisha Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, Ikulu, Dar es Salaam leo, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema) amemnyooshea kidole waziri huyo.
Kupitia
taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Lema ambaye ni Waziri Kivuli
wa Mambo ya Ndani, alisema wizara hiyo ni nyeti na muhimu kwa usalama
wa taifa hivyo Mwigulu anapaswa kuwa makini, mwangalifu na mwenye
utulivu.
“Ni
heshima kubwa uliyopewa na Rais, unapaswa kuwa makini, mwangalifu na
mwenye utulivu. Natarajia jambo la kwanza utakalofanya ni kutambua
kuwa na wingi wa silaha za kisasa kwa askari wetu si suluhisho la
ulinzi na amani katika taifa letu, bali haki na matumaini ya wananchi
ndiyo msingi madhubuti wa amani na utulivu wa nchi.
“Polisi
wetu na askari magereza wanaishi maisha magumu, mishahara haitoshi
wanahitaji uelewa wako juu ya maisha yao na kazi zao.
“Umeteuliwa wakati Serikali kupitia jeshi la polisi inatumia nguvu zote kukandamiza na kuangamiza demokrasia.
“Vyama
vya siasa vimezuiwa kufanya mikutano ya hadhara nchi nzima kwa sababu
ambazo hazina msingi wowote kinyume cha sheria na Katiba ya nchi, huku
pia uhuru wa maoni, habari na taarifa ukiwa shakani,” alisema.
Alisema
taifa linatarajia Waziri Mwigulu atakuwa mshauri mzuri wa Rais
Magufuli kuhusu masuala hayo pamoja na wajibu wa polisi katika
demokrasia kwa sababu kuitia shaka demokrasia ni kuharibu ustawi wa
jamii nchini.
Alimshauri
Mwigulu kutafuta waraka wa hotuba ya kambi ya upinzani kwa wizara hiyo
iliyozuiliwa kusomwa bungeni kwa sababu ina mambo mengi ambayo yanaweza
kumsaidia.
“Kuna
mambo mengi tulilieleza katika hotuba yetu… ni vema ukaitafuta hotuba
hiyo na ukatazama kwa makini mambo ambayo yalizuiwa kusomwa na uone
namna utakavyowajibika juu ya mambo hayo.
“Hapo ndipo unapaswa kuanzia. Na wananchi wanasubiri kukupima katika hilo.
“Hata
hivyo, ninakutakia kila la heri katika wajibu wako huu mpya, ninafahamu
changamoto za wizara hii hasa wakati huu ambao mauaji ya binadamu na
ugaidi ni tishio duniani na Afrika Mashariki,” alisema.
Pamoja
na kumwapisha Waziri Mwigulu leo, Rais Magufuli pia anatarajiwa
kumwapisha Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Charles Tizeba.
Kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu ndiye alikuwa Wazira wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini