Mbunge Ataka Walawiti na Wabakaji Wahasiwe. | nyula blog

Habari Kila Pande

Breaking News
Loading...

Friday, May 6, 2016

Mbunge Ataka Walawiti na Wabakaji Wahasiwe.

MBUNGE wa Viti Maalumu, Angelina Malembeka (CCM) ametaka watu wanaohukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa la ubakaji na ulawiti, wahasiwe ili wawapo gerezani wasiendeleze tabia hizo.

“Tumeshaona wanaohukumiwa kifungo cha maisha, wakiwa huko gerezani wanaendeleza vitendo vya kulawitiana, kwa nini sasa wasihasiwe?” Alihoji. 
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe, wakati akimjibu jana alisema, “siwezi kuwa na jibu kwa sababu Bunge ndilo linalotunga sheria, mbunge aje na wazo lake hapa bungeni lipitishwe kama sheria sisi Serikali hatuwezi.”

Akitoa ufafanuzi zaidi juu ya hali ya ubakaji na ulawiti, Dk Mwakyembe alisema kila siku nchini kunaripotiwa matukio 19 ya kubakwa na kulawitiwa.

Alisema hali ni mbaya sana na sasa kuna mashauri 2,031 yaliyoripotiwa mahakamani katika kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu. 
Kati yake mashauri hayo, 111 yameshakamilishwa kwa kuhukumiwa ambapo watu 99 wamefungwa, watuhumiwa 18 wameachiwa huru kwa kukosa ushahidi na kesi 1,920 hazijakamilika.

Akijibu swali la msingi la mbunge huyo aliyehoji mpango wa Serikali kuhakikisha kesi za kubakwa na kulawitiwa hazimalizwi kifamilia, Dk Mwakyembe alisema kumalizwa kwa kesi kifamilia kunachochea vitendo hivyo kuendelea katika jamii.

“Tatizo la kuficha ushahidi na kumaliza kesi hizo kifamilia, haliwezi kumalizwa na vyombo vya dola peke yake bila ushirikiano na wananchi wanaoishi na watuhumiwa. Hivyo Serikali imekuwa ikitoa elimu kwa umma kuwa kuficha ushahidi na kuyamaliza matukio hayo ya jinai kifamilia si kosa peke yake, bali vilevile utaratibu huo unachochea vitendo hivyo kuendelea katika jamii,” alifafanua.

Ili kuweka mazingira rafiki kwa waathirika na wananchi wenye taarifa au ushahidi wa aina hiyo, alisema Serikali imeanzisha madawati ya jinsia katika vituo mbalimbali vya Polisi yanayopokea taarifa mbalimbali kutoka kwa wananchi na kuliwezesha Jeshi la Polisi kuendesha upelelezi kwa ufanisi.

“Pindi tukio la kubaka au kulawiti litakaporipotiwa, upelelezi hufanyika na mtuhumiwa kufunguliwa mashitaka mara moja, kwa utaratibu huu Serikali inahakikisha kuwa matukio haya hayamalizwi nje ya utaratibu wa haki jinai,” alisema.

Sheria ya Kanuni ya Adhabu sura ya 16 imeweka adhabu ya kifungo cha maisha kwa mtu yeyote anayekutwa na hatia ya kumbaka msichana. Pia sheria imeweka adhabu ya kifungo cha miaka 14 kwa kosa la kulawiti.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini

google+

linkedin