Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewasimamisha kazi wakuu
wawili wa idara katika manispaa mbili kwa tuhuma za kushindwa kutoa
maelezo kuhusu watumishi hewa katika idara zao, huku wakiendelea
kuidhinisha mishahara yao kwa miaka mingi.
Makonda aliwataja
watumishi hao waliosimamishwa kazi kuwa ni Mkuu wa Idara ya Utumishi wa
Manispaa ya Ilala, Francis Kilawe na Mkuu wa Idara ya Afya Temeke,
Syrivia Mamkwe na kuagiza uchunguzi dhidi ya tuhuma zao ufanyike haraka.
Kiongozi huyo alichukua uamuzi huo baada ya hivi karibuni
kuwaapisha wakuu wa idara kutoka manispaa tatu ili kusema ukweli na
kuwapa wiki moja kuhakiki watumishi hewa katika maeneo yao ya kazi.
Makonda
alisema hadi kufikia jana, jumla ya watumishi hewa 39 waligundulika na
kufikisha 248 kutoka 209 wa takwimu za awali.
Kati yao, 26 wanatoka
Ilala, wawili (Kinondoni) na 11 (Temeke) na kulisababishia jiji hilo
kupata hasara ya zaidi Sh3 bilioni.
“Kilawe
ameshindwa kujieleza kuhusu watumishi hewa 11 ambao hajui wako wapi,
lakini wanapokea mishahara tangu mwaka 2010.Huku yeye akisaini mishahara
yao,” alisema Makonda.
Makonda
ambaye pia aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni aliongeza kuwa
Mamkwe alishindwa kujieleza walipo watumishi hewa wawili ambao bado
wanaendelea kupata mishahara huku akiwa kiongozi wa idara husika.
Kutokana
na hali hiyo, Makonda amewaongezea wiki mbili maofisa wanaochunguza
suala hilo ili kuwabaini zaidi watumishi hewa kwa madai kuwa bado
wanaonekana katika mfumo wa kupokea malipo kutoka Hazina kwenda katika
manispaa.
“Huu ndiyo mkutano wangu wa mwisho kwenu.Wiki hizi
mbili zikiisha tutaanza uchunguzi dhidi yenu na tukibaini watumishi hewa
katika idara yako utawajibishwa ,” alisema Makonda ambaye pia ni Katibu
wa Chipukizi na Uhamasishaji wa UVCCM.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini