Serikali
imetaja manufaa ya mradi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka
Uganda hadi Tanzania kuwa miongoni ni kuongezeka kwa uwekezaji wa fedha
za kigeni na fursa za ajira.
Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo aliliambia Bunge jana
kuwa Aprili mwaka huu, Tanzania ilisaini Makubaliano ya Awali (MoU) na
Serikali ya Uganda kwa ajili ya ujenzi wa bomba hilo kutoka Hoima,
Uganda hadi Bandari ya Tanga.
Alisema bomba hilo litakuwa na urefu wa kilometa 1,443 ambazo kati ya hizo, kilometa 1,115 zitakuwa upande wa Tanzania.
“Bomba hilo litakuwa na uwezo wa kusafirisha mapipa 200,000 ya mafuta ghafi kwa siku,” alisema
Profesa Muhongo akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara
yake kwa mwaka 2016/17 yanayofikia Sh 1,122,583,517,000.
Aliyataja
manufaa ya bomba hilo kwa Tanzania kuwa ni kuongezeka kwa ukusanyaji wa
mapato kupitia Bandari ya Tanga, tozo ya kupitisha mafuta ghafi kwenye
bomba na ajira za kudumu kwa Watanzania 1,000 na 10,000 za muda.
Alisema
majadiliano ya utekelezaji wa mradi huo kati ya Serikali za Tanzania,
Uganda, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) pamoja na
kampuni za Total (Ufaransa), CNOOC (China) na Tullow (Uingereza)
yameanza.
Alisema
katika kuimarisha ushirikiano wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki,
Serikali ya Uganda imealika nchi za Burundi, Kenya, Rwanda na Tanzania
kushiriki katika uwekezaji wa mradi wa ujenzi wa kiwanda cha kusafisha
mafuta ghafi nchini Uganda.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini