Kauli
ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kuwa baadhi ya wafanyabiashara
wameficha sukari ili kutengeneza uhaba sokoni utakaopandisha bei ya
bidhaa hiyo, imedhihirika baada ya baadhi ya wafanyabiashara hao kuanza
kukamatwa wakiwa na vidhibiti.
Kutokana
na hali hiyo iliyosababisha bei ya bidhaa hiyo kuanza kupanda, Waziri
Mkuu Majaliwa, alitangaza uamuzi wa Serikali kuagiza sukari yake nje
itakayouzwa kwa bei elekezi kwa wananchi ya Sh 1,800 kwa kilo, ili
kuzuia ongezeko hilo haramu la bei.
Akizungumza
na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Wilaya ya Singida, Saidi Amanzi
alitangaza polisi kuwashikilia wafanyabiashara wawili wa mjini hapa kwa
tuhuma za kukutwa na zaidi ya mifuko 655 ya sukari, sawa na tani 24.3,
ikiwa imekifichwa kwenye stoo zao.
Kwa
mujibu wa Amanzi, wafanyabiashara hao walikamatwa kwenye msako
ulioendeshwa na watendaji wa Halmashauri ya Manispaa Singida pamoja na
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya.
Amanzi
alisema kuwa msako huo uliendeshwa baada ya kupata taarifa za siri kuwa
kuna baadhi ya wafanyabiashara waliokuwa wameficha sukari, ili waje
kuiuza kwa bei ya juu kwa wateja wao kwa kisingizio kuwa kuna uhaba
mkubwa wa bidhaa hiyo.
“Katika
msako huo, tumemnasa Mohamed Alute Ally (44), mfanyabiashara wa eneo la
Unyankindi aliyekutwa na mifuko 335 ya kilo 25 kila mmoja na Yusufu
Suleiman (39), mfanyabiashara wa eneo la Minga katika manispaa ya
Singida aliyepatikana na mifuko 320 ya kilo 50,” alisema.
Mkuu
huyo wa wilaya ametoa mwito kwa wafanyabiashara wote kuacha kuficha
bidhaa zote muhimu, ikiwemo sukari na mchele, bali waiuze kwa bei halali
kwa wateja wao.
Wakati
huo huo, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Joseph Mchina, amesema msako
mkali unaohusisha kikosi kazi maalumu pamoja na Kamati ya Ulinzi na
Usalama utaendelea kwa nguvu zote na kusisitiza kuwa kuhodhi bidhaa kwa
sababu yoyote ile ni kosa la uhujumu uchumi.
Mmoja
wa Wakala wa Kiwanda cha Sukari cha TPC Moshi Mjini, Salim Nagji,
amesema mfuko mmoja wa sukari huuzwa Sh 92,650 lakini tangu sukari
iadimike mfuko unauzwa kati ya Sh 115,000 na Sh 120,000 huku kilo moja
ikiuzwa kati ya Sh 2,400 na Sh 2,800 kwa kilo kinyume na bei elekezi ya
Sh 1,800.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini