Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali imepokea ushauri uliotolewa na
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT- Wazalendo) wa kuishitaki Benki
ya Standard (ICBC) ya Uingereza, kuhusu ufisadi uliofanyika katika
mkopo wa Dola za Marekani milioni 600 (Sh trilioni 1.2) ambazo Serikali
ilikopa kwa kutumia hati fungani.
Ushauri
mwingine uliotolewa na Zitto ambao Waziri Mkuu amesema Serikali
itaufanyia kazi ni kuhusu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru), kuwafikisha mahakamani wahusika wa sakata la akaunti ya
Tegeta Escrow, ili sheria ichukue mkondo wake.
Zitto
alitoa ushauri huo bungeni mjini Dodoma juzi, wakati akichangia hotuba
ya bajeti ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora,
iliyowasilishwa na Waziri Angela Kairuki.
Hotuba
ya bajeti ya ofisi hiyo inajadiliwa na wabunge pamoja na ile ya Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi),
iliyowasilishwa na Waziri wake, George Simbachawene.
Akizungumza
na wanahabari jana, Waziri Mkuu alisema, hoja ya Zitto ina mashiko na
akiwa msimamizi wa shughuli za Serikali bungeni, atahakikisha ushauri
huo unafanyiwa kazi.
“Sisi
kama Serikali tutaifanyia kazi na pale tutakapoona tumefikia katika
hatua ya kutoa taarifa kwa umma kuhusu utekelezaji wa ushauri huo,
tutafanya hivyo,” alisema.
Benki ya Standard
Kuhusu
Benki ya Standard ya Uingereza, Zitto alisema mkopo huo wenye riba
yenye kuweza kupanda na kushuka, umeanza kulipwa Machi mwaka huu na
utalipwa mpaka mwaka 2020 kwa mikupuo tisa inayolingana.
Alisema,
ifikapo mwaka 2020, Tanzania itakuwa imelipa deni hilo pamoja na riba
ambayo ni Dola za Marekani milioni 897 sawa na Sh trilioni 2, huku
akidai kuwa mkopo huo umegubikwa na ufisadi na wapo baadhi ya Watanzania
wamefikishwa mahakamani kuhusu sehemu ya mkopo huo.
Alisema
Takukuru katika kesi hiyo, inasaidiwa na wataalamu kutoka Uingereza
katika kesi inayohusu Benki ya Uingereza, huku kukiwa na Watanzania
walioandika ‘petition’ kutaka Benki ya Standard kuchunguzwa wakitaka
ukweli wote kujulikana.
Escrow
Kuhusu
IPTL Tegeta Escrow, Zitto alisema mwaka 2014, Takukuru iliijulisha
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kwamba ilikuwa inachunguza
na kumaliza uchunguzi kuhusu miamala ya kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow
Benki Kuu ya Tanzania kwenda Benki ya Stanbc Tanzania.
Alisema katika taarifa zote ambazo Takukuru inatoa kuhusu kesi za ufisadi, hakuna mahali inapozungumzia maendeleo ya suala hilo.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini