Wajumbe wa Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira wamekerwa na kiwango
cha bajeti ya Sh95. 6 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya Wizara ya
Viwanda, Biashara na Uwekezaji, wakisema haionyeshi malengo ya Tanzania
kuelekea kuwa nchi ya viwanda.
Wabunge walisema hayo baada ya
Waziri Charles Mwijage kuwasilisha taarifa ya makadirio ya mapato na
matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa 2016/17 mbele ya kamati.
Waziri
Mwijage alisema kati ya fedha hizo, Sh 53.5 bilioni (sawa na asilimia
56), zimetengwa kwa matumizi ya kawaida wakati Sh42.1 bilioni (asilimia
44) ni kwa ajili ya maendeleo.
Mbunge wa viti maalumu (Chadema),
Hawa Subira alisema wakati wa kujadili taarifa hiyo kuwa kiwango hicho
kinaonyesha wazi jinsi Serikali isivyo na nia ya kufufua viwanda kama
alivyoahidi Rais John Magufuli.
“Homa ya Magufuli inawaogopesha.
Nakuonea huruma waziri (kwa kuwa) unaonyesha kabisa kuwa una nia njema,
lakini kwa mtindo huu lazima uumwe,” alisema Subira.
“Tafuteni
panadol tuwasaidieni. Tunataka nchi hii kweli iwe ya viwanda. Hatuwezi
kufanya kazi namna hii watu mmejaa uoga hata kupanga bajeti ya kueleweka
mnashindwa au mkikaa mnaogopa kurekodiwa,” alisema.
Mbunge wa
Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema alisema nchi kuwa ya viwanda na
biashara inawezekana, lakini Serikali inapaswa kudhihirisha kwa vitendo
badala ya maneno kwa kuwa wizara hiyo ilipaswa kutengewa fedha za
kutosha kuonyesha njia ya kuelekea kwenye malengo yaliyokusudiwa, kama
kuruhusu safari za nje ya nchi kwa maofisa wa wizara kwa nia njema.
“Lakini
kuna mambo yamekuwa yakifanyika ya ajabu. Mimi naweka mambo ya siasa
pembeni. Serikali iangalie upya hii bajeti, lakini pia huo mradi wa
China Logistics Centre hauna msaada kwa nchi badala yake utaua hata
viwanda vidogo vidogo vilivyopaswa kusaidiwa kuinuka. Hatuwezi kuifanya
Dar kuwa Dubai wakati viwanda vya ndani havijaimarishwa,” alisema.
Kwa
upande wake mbunge wa Nkenge(CCM), Dk Diodorus Kamala alisema wakati
mwingine Serikali imekuwa ikiwapa wapinzani kauli kutokana na mambo
inayofanya.
Alisema kiwango hicho cha fedha hakiendani hata na taarifa
aliyoiyoa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango hivi karibuni
alipowasilisha mapendekezo ya mpango wa bajeti.
“Fedha ni ndogo
wakati tunatakiwa tujikomboe kwa kupiga hatua za kimaendeleo kutoka hapo
tulipo. Mfano naona wizara imeridhika kuwa pale kwenye jengo la Water
Front, badala ya bajeti hii kueleza mpango wake wa kujenga ofisi ya
kujitegemea ili kusaidia hata kupunguza matumizi,” alisema.
Akijibu
hoja hizo, Mwijage alisema haoni tatizo kwa kiwango cha bajeti
alichotengewa kwa kuwa malengo ya wizara yake kwa mwaka huu wa fedha
pamoja na mambo mengine ni kuboresha mazingira ya viwanda vilivyopo
kisha mwaka ujao ndipo watajikita kujenga vipya.
“Ninachokiona
hapa ni kwamba wengi wanataka kuona nchi inakuwa hivyo leo, kumbe
tunatakiwa kuanzia kwa kuboresha mazingira ya hivi vilivyopo kwani vingi
vinazalisha chini ya asilimia 50 kutokana na vikwazo mbalimbali ikiwamo
miundombinu duni,” alisema.
Katika mapendekezo ya mpango wa
bajeti ya 2016/17, Serikali imeweka fedha nyingi katika kuboresha
miundombinu ya usafiri kama reli, barabara na viwanja vya ndege,
uzalishaji wa nishati ya uhakika, hasa umeme unaotokana na gesi na makaa
ya mawe na kuboresha rasilimali watu kwa ajili ya kuweka mazingira
wezeshi ya kukua kwa viwanda.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini