Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) leo anawasilisha bungeni
ripoti ya mwisho ya ukaguzi wa hesabu za serikali ya mwaka 2014/15.
Ingawa
haijajulikana rasmi nini kilichomo ndani yake, baadhi ya watu
waliohojiwa wanatarajia CAG kubaini mchwa wanaotafuna fedha za umma na
namna ya kukabiliana nao.
Aidha wengine wanatarajia taarifa ya hali bora zaidi ya usimamizi wa fedha za umma kuliko kipindi cha nyuma.
Ripoti hiyo awali ilikuwa imepangwa kuwasilishwa bungeni mwishoni mwa wiki (Aprili 22) kabla ya kuahirishwa hadi leo.
“Ni kweli CAG atawasilisha ripoti kesho (leo) bungeni, ”Naibu Katibu wa Bunge na Utawala, Joel Joel alithibitisha juu ya kuwasilishwa kwa ripoti hiyo leo.
Miongoni
mwa wabunge waliozungumza na mwandishi wa habari hizi, wamesema
wanatarajia CAG kuonesha mambo mazuri kwa maana ya taasisi zilizofanya
vizuri katika usimamizi wa fedha za umma lakini pia mambo mabaya.
“Lazima ripoti itaibua madudu maana walizoea (watendaji serikali) kana kwamba hapakuwapo na serikali,”
alisema Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy na kusisitiza kuwa
pamoja na wabunge wenzake, watamsaidia Rais John Magufuli kupambana na
ubadhirifu serikalini.
Keisy
alisema akiwa mbunge, anaamini pamoja na wenzake, wanachosubiri ni
kuona ripoti hiyo na kuhakikisha wanaohusika na kuchezea fedha za
serikali, kabla ya kufikishwa mahakamani, wanarudisha fedha hizo.
“Atakachosema CAG sisi tutakuwa tayari kusimama kusaidia Rais aendelee kupambana na ubadhirifu,” alisema.
Kwa
upande wake, Mbunge wa Mbinga Vijijini, Martin Msuha, alisema ripoti
hiyo ni muhimu katika usimamizi wa serikali na inategemewa kuwa na mambo
mazuri na mabaya kwa maana ya majipu ambayo yatapaswa kutumbuliwa.
Mbunge
wa Bukoba Vijijini, Jasson Rweikiza alisema matarajio waliyo nayo ni
kwamba ubadhirifu na wizi utakaoibuliwa na ripoti hiyo utashughulikiwa
mara moja.
“Kama
kuna ubadhirifu, mishahara hewa na wizi vyote vishughulikiwe...kama
kuna ubadhirifu na wizi wowote, mwizi mahali pake ni jela,” alisema Rweikiza akishutumu uwapo wafanyakazi hewa katika halmashauri yake.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini