Waziri
Mkuu mstaafu, Dk. Salim Ahmed Salim, ameshangazwa na uamuzi wa Tume ya
Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kufuta uchaguzi visiwani humo.
Amesema
jumuiya za kimatifa zilishtushwa na uamuzi huo.Salim amesema kutokana
na hali hiyo, kinachotakiwa hivi sasa ni haki itendeke kwa kila kila
upande kukaa na kutafuta suluhisho la kudumu.
“Tanzania haijazoea migogoro ya siasa jambo ambalo si jema katika sura ya kimataifa,” alisema.
Mwanadiplomasia
huyo wa kimataifa ametoa kauli hiyo,baada ya Mwenyekiti wa ZEC, Jecha
Salim Jecha, kutangaza kufuta matokeo ya uchaguzi huo Oktoba 28, mwaka
jana.
Siku chache zilizopita, Jecha alitangaza kuwa uchaguzi huo unatarajiwa kurudiwa Machi 20 mwaka huu.
Mwanadiplomasia
huyo wa kimataifa aliwahi kushika nafasi mbalimbali ikiwamo ya Katibu
Mkuu wa Umoja wa Nchi za Afrika (OAU) ambayo kwa sasa inatambulika
kama Umoja wa Afrika (AU).
Alisema
hatua ya kufutwa uchaguzi wa Zanzibar ni jambo lililowashangaza wengi
kwa kuwa uchaguzi ulifanyika kwa amani na utulivu, huku waangalizi wa
ndani na nje wakiusifia katika ripoti zao.
“Ni
hatua ambayo imewashangaza wengi…imeibua sintofahamu kubwa katika nchi
yetu kwa sababu uchaguzi uliopita Tanzania ilipata sifa,baada ya
uchaguzi kufanyika kwa amani na utulivu. Lakini kitendo cha kufutwa
kumewashangaza wengi na bado suala hili halieleweki.
“Pia
hili jambo sidhani kama ni la mtu mmoja…sidhani kama ni la Jecha peke
yake. Huu si mustakabali mzuri kabisa, Zanzibar ni nchi ndogo, lakini
ina historia kubwa kisiasa hivyo juhudi za pamoja zifanyike kutatua
mgogoro huu kwa matakwa ya Watanzania kwa ujumla.
“Viongozi
wasisitize amani na utulivu na katika hili la Zanzibar kwa kweli haki
itendeke na waache ushabiki wa vyama iwe CCM au Upinzani, wote waweke
ushabiki pembeni na watatue mgogoro huu kwa mustakabali wa Wazanzibari
na Watanzania kwa ujumla,” alisema Dk. Salim.
Alisema
ingawa viongozi mbalimbali wamekutana na kufanya mazungumzo bila kupata
suluhu,pande zote ziendelee kukutana hadi suluhu ya pamoja ipatikane.
Salim,
alisema kuendelea kuachia hali hiyo iendelee kuna hatari ya kujenga
uhasama zaidi hivyo ni vema viongozi wafikirie zaidi masilahi ya
Zanzibar.
“Nchi
ipo katika hali mbaya, migogoro iko kila pahala,Watanzania hatujazoea.
Jambo hili la Zanzibar likiendelea litazaa matatizo makubwa katika Taifa
letu.
“Waliangalie kwa uzito hata kama tarehe ya uchaguzi imetangazwa waendelee na mazungumzo,” alisema mwadiplomasia huyo wa kimataifa.
Dk.
Salim ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, alipoulizwa kama
Kamati Kuu ya chama tawala katika vikao vyake ilijadili suala la
Zanzibar, alisema limegusiwa ingawa haikuzungumzwa na ni nini
kifanyike.
“…japo
sikushiriki vikao vyote hivi karibuni kwa sababu nilikuwa katika
majukumu mengine, jambo hili limezungumzwa japo halikugusiwa nini
kifanyike.
“Jambo
hili, linastahili kupewa kipaumbele hata katika vikao vya Kamati ya Kuu
ya CUF (Chama cha Wananchi) na vyama vingine kwa sababu madhara
yakitokea yataathiri kila upande,” alisema.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini