WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewasili mkoani Kilimanjaro na kufanya ziara
kushtukiza kwenye hospitali ya rufaa ya Mawenzi ambayo ni hospitali ya
mkoa huo.
Waziri
Mkuu Majaliwa ambaye mara baada ya kuwasili Ikulu ndogo ya Moshi mjini
jana jioni (Jumamosi, Januari 30, 2016) alipangiwa kupokea taarifa ya
mkoa huo, alimweleza Mkuu wa mkoa huo kwamba anataka kufanya ziara
katika hospitali hiyo na kuwaomba radhi watendaji waliokuwa wanasubiri
taarifa ya mkoa iwasilishwe.
“Mheshimiwa
Waziri Mkuu ameamua kufanya ziara katika hospitali ya rufaa ya Mawenzi
ambayo ni hospitali yetu ya mkoa na atakuja kupokea taarifa ya mkoa wetu
tukishatoka huko,” alisema Mkuu wa mkoa huo, Bw. Amos Makalla.(VICTOR)
Mara
baada ya kuwasili hospitalini, Waziri Mkuu alielekeza apelekwe kwenye
chumba cha upasuaji (theatre) huku akimuuliza maswali kadhaa Mganga
Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Bingileki Lwezaula.
Katika
chumba cha upasuaji ilibainika kuwa kuna vyumba vitatu vya kufanyia
upasuaji lakini kinachotumika ni kimoja tu kwa sababu vingine havina
dawa za kulaza wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji (anesthesia) licha ya kuwa
jengo la upasuaji lina mwaka sasa tangu lilipozinduliwa Februari, 2015
na Rais Mstaafu Jakaya Kikwete.
Akiwa
katika wodi ya utabibu ya wanawake, Waziri Mkuu alipokea malalamiko
kutoka kwa wagonjwa juu ya kukosekana kwa dawa hospitalini hapo. Afisa
Muuguzi wa wodi hiyo, Bi. Anjela Mwakalile alisema wametuma maombi ya
kupatiwa dawa kutoka MSD lakini bado hazijafika.
Hali hiyo
ilijitokeza pia kwenye wodi ya watoto. Akizungumza na wazazi wa watoto
aliowakuta wamelazwa, mama mmoja alimweleza Waziri Mkuu kwamba sera ya
Taifa inasema watoto wachanga hadi walio na miaka mitano wanapaswa
kupata matibabu bure, lakini wao hapo hospitalini wanalazimika kununua
dawa.
Waziri
Mkuu alimtaka Mganga Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Mtumwa Mwako kubadili haraka
mfumo wa uagizaji wa dawa baada ya kupokea maelezo ya Dk. Lwezaula
kwamba wametuma maombi MSD tangu miezi miwili iliyopita lakini hadi sasa
hawajaletewa dawa walizoomba.
“RMO ni
kwa nini hamuwezi kuagiza dawa nyingi (bulk) kwa magonjwa ambayo mnajua
yanajirudia mara kwa mara ili wagonjwa weu wasipate usumbufu? Hii ni
hospitali ya mkoa na mgao wa dawa unaopaswa kuja hapa ni wa level ya
mkoa? Haiwezekani mnafanya hivyo ili wagonjwa wajinunulie dawa kutoka
kwenye maduka yenu?,” alihoji Waziri Mkuu.
“Hii
hospitali ni kubwa kuliko idadi ya wagonjwa wanaofika kutibiwa hapa na
hii ni kwa sababu wengi wao wanaishia kwenye hospitali za wilaya. Kwa
hiyo mlipaswa kuwa na dawa za kutosha. Wodini nimekuta wagonjwa wachache
katika wodi nilizopita, ina maana mna ahueni hapa... mnao madaktari wa
kutosha, wataalamu 12, lakini ni kwa nini hakuna dawa za kutosha?”
alihoji. Wakati akitoka wodi ya watoto, kijana mmoja aliyejitambulisha
kwa jina la Bakari Hussein ambaye anauguza mgonjwa wake hospitalini hapo
alimweleza Waziri Mkuu kwamba dawa pekee wanayopatiwa kwenye hospitali
hiyo ni paracetamol tu.
“Hapa
dawa ya bure pekee unayopata ni paracetamol tu. Dawa nyingine zote
unaandikiwa ukanunue maduka ya nje. Na ukizipata ni kati ya sh. 60,000/-
hadi 70,000/- kwa mkupuo. Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemuagiza
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Bw. Severine Kahitwa apeleke
maombi ya kupatiwa mafundi wa mashine zaxray haraka iwezekanavyo kwa
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto.
Waziri
Mkuu amefikia uamuzi huo baada ya kukuta mashine kubwa kwenye chumba cha
mionzi cha hospitali haifanyi kazi na inayofanya kazi ni ndogo haiwezi
kufanya baadhi ya vipimo.
Akitoa
maelezo mbele ya Waziri Mkuu, Mkuu wa kitengo cha Radiolojia, Dk.
Ephraim Minja alisema: “Tuliambiwa spare parts zimekwama bandarini, na
vifaa hivyo vikipatikana vitaweza kutatua tatizo lililopo.”
Alipoulizwa
na Waziri Mkuu kabla ya mashine ya kuharibika alikuwa akihudumia
wagonjwa wangapi, Dk. Minja alisema kwa wastani alikuwa akihudumia
wagonjwa 60 hadi 70. “RAS fuatilia mafundi kwa Katibu Wizara ya Afya.
Hii ni hospitali kubwa tena ya Serikali kwa hiyo haiwezekani wagonjwa
waje hapa na kuambiwa waende kupata vipimo mtaani,” alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, JANUARI 31, 2016.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini