Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepokea kwa furaha uteuzi
uliofanywa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mhe. Ban Ki-Moon wa
kumteua Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais Mstaafu wa awamu ya
nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa mmoja wa wenyeviti wa jopo
la ushauri la ngazi ya juu kuhusu Afya ya Mama na Mtoto (Every Woman,
Every Child) Duniani.
Kwa
niaba ya Serikali, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto na kwa niaba yangu binafsi napenda kuchukua fursa hii kumpongeza
kwa dhati Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa uteuzi huu.
Wakati
wa uongozi wa Serikali yake ya awamu ya nne, Mhe. Dkt Jakaya Kikwete
amekuwa mstari wa mbele kitaifa na kimataifa katika kusimamia na kutetea
huduma bora za afya ya mama na mtoto.
Mwaka
2005, mara baada ya kuingia madarakani Mhe. Dkt Jakaya Kikwete aliagiza
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuandaa Mpango wa Maendeleo wa Afya
ya Msingi (MMAM) akiwa na nia ya kusogeza huduma za afya karibu na
wananchi, hususan huduma ya afya ya uzazi na mtoto. Kutokana na jitihada
zake hizo, vituo vya kutolea huduma za afya vya umma viliongezeka
kutoka 5,172 mwaka 2005 hadi 7,247 mwaka 2015.
Mwaka
2007, Mhe Dkt. Jakaya Kikwete aliungana na Waziri Mkuu wa Norway Mhe.
Jens Stoltenberg na viongozi wengine wa kimataifa kuanzisha Mtandao wa
Viongozi wa Dunia wa kutoa msaada wa kisiasa katika ngazi ya juu kabisa
na kufanya uragibishaji (advocacy) kwa ajili ya malengo ya milenia
namba 4 na 5 yanayohusu kupunguza vifo vya watoto na wanawake
wajawazito. (Network of Global Leaders Advocating for MDG4 and 5).
Mwaka
2008, Mhe Dkt. Jakaya Kikwete alizindua Mpango Mkakati wa Taifa wa
Kuongeza Kasi ya Kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vya watoto
wachanga (Road Map to Accelerate Reduction of Maternal Newborn and Child
Health 2008-2015).
Mwaka
2014 alizindua Mpango Mkakati ulioboreshwa kupunguza vifo vitokanavyo
na uzazi na vya watoto (Sharpened One Maternal Newborn and Child Health
Plan 2014-2015).
Sambamba
na uzinduzi wa mpango mkakati huo, pia alizindua kadi maalum ya
kutathmini utekelezaji katika afua za kupunguza vifo vitokanavyo na
uzazi na vya watoto.
Kadi hii aliikabidhi kwa Wakuu wa Mikoa wote nchini na kuwaagiza wasimamie kwa karibu na kuwa atafuatilia utekelezaji wake.
Mwaka
2010, Dkt. Jakaya Kikwete aliungana na Mhe. Ban Ki-moon wakati
anatangaza nia ya kuwa na mpango mkakati wa kimataifa wa afya ya
wanawake na watoto “UN Secretary General’s Strategy for Women’s and
Children’s Health 2010-15”.
Baada
ya mkakati huu kukamilika Desemba 2010, Mhe. Dkt. Kikwete aliteuliwa
na Mhe. Ban Ki-Moon kuwa Mwenyekiti Mwenza wa Tume ya Taarifa na
Uwajibikaji kwa ajili ya Afya ya Wanawake na Watoto “UN Commission on
Information and Accountability for Women’s and Children’s Health”.
Kazi
hii aliifanya kwa umahiri na weledi mkubwa kwa kushirikiana na
Mwenyekiti mwenza aliyekuwa Waziri Mkuu wa Canada, Mhe. Stephen Harper.
Tume
hiyo iliwasilisha ripoti yake kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa mwezi
Septemba, 2011. Ripoti hii iliwezesha nchi wanachama wa Umoja wa
Mataifa kuchukuwa jitihada mbalimbali za haraka na za makusudi za
kuboresha afya ya mama na mtoto katika nchi zao.
Baada
ya hapo, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete aliendelea kuwa mtetezi wa afya
ya akina mama na watoto, chanjo, kudhibiti malaria na UKIMWI ndani na
nje ya Tanzania.
Katika
kipindi cha uongozi wake, nchi yetu imepata mafanikio makubwa katika
kutimiza malengo ya milenia hususani lengo namba 4 linalolenga kupunguza
vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano, ambapo vifo
vimepungua kutoka 112 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2005 hadi 81 kwa
kila vizazi hai 1,000 mwaka 2010.
Aidha,
mwaka 2013 ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu vifo vya watoto ilionyesha
kuwa Tanzania imefikia vifo 54 kwa kila vizazi hai 1,000 na hivyo
kufikia lengo la Milenia namba 4 hata kabla ya mwaka 2015.
Vifo
vya akina mama vitokanavyo na uzazi vimepungua kutoka 578 kwa kila
vizazi hai 100,000 mwaka 2005 hadi 454 kwa kila vizazi hai 100,000
mwaka 2010. Na kutokana na ripoti ya Umoja wa Mataifa ya mwaka 2014
tumefikia vifo 410 kwa kila vizazi hai 100,000.
Afya
ya mama na mtoto ni kipaumbele kwa Serikali ya Awamu ya Tano
inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Serikali kupitia
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto itaendeleza
juhudi hizi na kuhakikisha tunapiga hatua kufikia Malengo Endelevu ya
Kimataifa (Sustainable Development Goals 2030).
Tumedhamiria
kuwapa uhakika kina mama wa Tanzania wa kutopoteza maisha yao
wanapotekeleza haki yao ya msingi ya uzazi. Tutahakikisha tunapunguza au
kumaliza kabisa tatizo la vifo vya wanawake wajawazito na watoto
wachanga. Chini ya Kauli Mbiu ya ‘Hapa Kazi tu” ni dhahiri kuwa hili
linawezekana.
Pia,
tunaahidi kumpa ushirikiano Mhe. Rais Mstaafu Dkt Jakaya Kikwete katika
jukumu hilo alilopewa ambalo ni heshima kubwa kwa Taifa letu.
Tunamtakia kila la kheri katika utekelezaji wa majukumu yake.
Imetolewa na:
Ummy A. Mwalimu (Mb.)
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Dodoma
24 Januari 2016.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini