Ni
wiki nyingine tulivu kabisa tunakutana kupitia safu hii ambayo pamoja
na mambo mengine tunaelimishana na kukumbushana juu ya mambo mbalimbali
yanayogusa maisha yetu ya kila siku.
Mpenzi msomaji wangu, leo nitazungumzia
upendo unavyoweza kuwa silaha kwa adui yako ambaye mara nyingi amekuwa
akikupa hofu na wakati mwingine kuhisi ana dhamira ya kukufanyia mabaya.
Nimeamua kuandika makala haya baada ya
kuona na kusikia kesi nyingi juu ya watu kuishi maisha yaliyojaa hofu ya
kudhurika kwa visasi na vijicho vya wabaya wao.
Hakuna ubishi katika mtazamo wa dunia
kwamba kuna maisha chanya na hasi ambayo yanamzunguka mwanadamu. Lakini
ugumu anaoupata mwanadamu na pengine ndiyo ambao nataka kuuzungumzia leo
ni jinsi gani anaweza kuishi ndani ya mambo mema na mabaya.
Kama kilivyo kichwa cha habari hapo juu,
leo nimeona nijikite zaidi katika kutoa elimu ya namna ya kujikinga na
kumshinda mtu anayetaka kukuangamiza. Labda nitaje dhana tu ambazo
zinawaogopesha wengi katika maisha yao.
Kimsingi jamii inaogopa sana kurogwa,
kuuawa kwa nguvu za asili au kutendewa aina yoyote ya ukatili na watu
wabaya. Kuna kesi nyingi sana kwenye ndoa kuhusiana na kutaka
kuangamizana kwa uchawi na kutoana roho kwa silaha. Hali hii iko karibu
kila mahali anapoishi mwanadamu.
Katika maeneo ya kazi watu wanashindwa
kutekeleza majukumu yao kwa hofu ya kutendewa mabaya na wabaya wao,
lakini wapo ambao wamekufa kabisa kwa kufanyiwa hivyo na maadui zao,
inawezekana hata wewe unayesoma mada hii umeshasikia au kukumbwa na
kadhia ya adui yako.
Kimsingi hii ni changamoto isiyoepukika
katika maisha. Huwezi kuamua kuishi na watu wema tu na ukawakwepa wenye
roho mbaya na chuki zisizokuwa na sababu. Wale unaokula nao ndiyo wabaya
wako, methali ya Kiswahili inasema.
Unachotakiwa kufanya ni kujua tu nini cha kufanya ili umshinde adui yako na wewe uendelee kuishi maisha yako.
Muoneshe upendo adui yako
Watu wengi wamejikuta wakiwapa nafasi
adui zao kuwaangamiza kwa sababu hawajui nguvu ya upendo. Mara nyingi
upendo hutafsiriwa kama haki. Ninamaana kwamba kila apendaye anatenda
haki ambayo ina nguvu ya kumkinga na mabaya yote kutoka kwa hao
aliowapenda.
Zingatia jambo moja muhimu kuwa hatua ya
kwanza ya mtu kudhurika inaanzia kwenye hofu ambayo hukuzwa na mawazo
yake mweyewe, na siku zote mtu mwenye upendo hawezi kuhofu kutendewa
mabaya na watu aliowatendea wema na kuwapenda.
Kuwa na mawazo hayo pekee huweka kinga
thabiti ya mwili kukabili nguvu mbaya za asili zinazoelekezwa kwake, kwa
vile stahili ya kulipwa mabaya hukosekana moyoni.
Hutakiwi kumchukia mtu ambaye unahisi ni
adui yako. Unachotakiwa kufanya ni kumpenda na kujipendekeza kwake, ili
yeye aone aibu ya kukufanyia ubaya. Usilipe ubaya kwake hata kama
ushahidi unaonesha kuwa yeye ndiye aliyekufanyia kitu kibaya.
Ukifanya hivi utakuwa umejiokoa na
shambulio la adui yako kwa kiwango kikubwa. Nasisitiza upendo! Wanawake
mlioolewa wapendeni wifi, wakwe zenu hata kama mtahisi wana chuki dhidi
yenu.
Ni hayo tu kwa leo, tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini