Makamu
wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameyataka Mashirika yasiyo ya
Kiserikali nchini (NGOs) yanayoshughulikia masuala ya wanawake na watoto
kujenga utamaduni wa kushirikisha wanaume katika kampeni za kumwinua
mtoto wa kike kwa lengo la kuleta mabadiliko yanayokusudiwa.
Mheshimiwa
Samia ametoa kauli hiyo jana kwenye hafla ya uzinduzi wa Binti club
iliyofanyika sambamba na harambee ya fadhili mtoto asome ya kuchangisha
fedha kwa ajili ya watoto 500 wa wilaya ya Kinondoni iliyoandaliwa na
Shirika lisislo la Kiserikali la Binti Foundation katika ukumbi wa PSPF
jijini Dar es salaam
Alisema
wanaume kama wakala wa mabadiliko wanapaswa kushirikishwa na wajue
ajenda ili wawe mabalozi wazuri katika kuzungumzia umuhimu wa kumwinua
mtoto wa kike kielimu, kiafya na kwenye masuala ya ujasiriamali.
"Tuwaingize
wanaume kama wakala wa mabadiliko, tuwashirikishe, wajue ajenda zetu
katika mapambano hayo. wanaume wanashikilia sehemu nyingi, watumie
nafasi hizo tulete mabadiliko," alisema Makamu wa Rais na kuongeza "Penye
mkusanyiko wa watu 100, ukiingiza wanaume 20, na wakajua madhumuni ya
mkusanyiko wetu, wataenda kushawishi wenzao 20,000 huko nje."
Aliipongeza
Taasisi hiyo ya Binti Foundation kwa kuunga mkono jitihada za serikali
katika suala la elimu kwani safari ya mtoto wa kike ya kupata elimu
inakuwa na ugumu zaidi kuliko wanaume kutokana na kukabiliwa na
changamoto mbalimbali zikiwemo za mila potofu, hali ya uchumi katika
familia na jinsi jamii inavyomwangalia kutokana na ujanajike wake.
"Tuna kazi kubwa ya kumtayarisha mtoto wa kike aweze kupambana na changamoto zinazomzunguka," alidokeza.
Mheshimiwa
Samia alitumia fursa hiyo kuelezea hatua mbalimbali zinazochukuliwa na
serikali katika kukabiliana na changamoto za elimu ikiwa ni pamoja na
kuondoa ada katika shule za msingi na sekondari, kuboresha ajira za
walimu pamoja na maslahi yao, kujenga mabweni kwa wasichana na kuondoa
tatizo la madawati ambapo amewashukuru Watanzania kwa kuchangia
madawati.
Aliwataka
wazazi kuwatunza watoto wao kwani ni zawadi kutoka kwa Mungu na
kuhakikisha wanapata elimu zote ya dini na ya dunia ili kuwajenga
kimaadili waweze kuwa raia wema. Mtendaji Mkuu wa Binti Foundation
Johari Sadik alimweleza Makamu wa Rais kuwa shirika hilo liliamua kuunga
mkono jitihada za serikali ili kuwawezesha watoto kumudu masomo yao na
hatimaye kufikia malengo yao.
"Kwa
hiyo ukiwa na fedha taslimu, ama vifaa kama vile kalamu, madaftari,
pedi, vyote tunapokea kwa ajili ya kusaidia watoto ambao malengo yao
yanaweza yasitimie kutokana na changamoto hizo," Kampeni hiyo ya fadhili
mtoto asome imeanzia kwa watoto 500 wanaoishi kwenye mazingira magumu
wa shule za msingi Mwananyamala, Hananasif, Kumbukumbu na Msasani
zilizoko katika wilaya ya Kinondoni, mkoa wa Dar es salaam.
Katika
hafla hiyo iliyopambwa na onesho la mavazi la watoto Makamu wa Rais
ambaye alikubali kuwa mlezi wa Binti Foundation aliahidi kusomesha
watoto 100 wakati mke wa Waziri Mkuu, Mary Majaliwa alitoa ahadi pia ya
kusomesha watoto 50.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
Dar es salaam
19/6/2016
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini