Naibu
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia Wambura,
ametoa siku saba kwa Meneja Rasilimali Watu wa Shirika la Utangazaji la
Taifa (TBC), Neema Mrindoko kujieleza sababu za kuandika jina lake
katika kiwanja cha shirika kilichopo Kisarawe mkoani Pwani.
Wambura
alitoa agizo hilo juzi alipotembelea kiwanja hicho kilichopo eneo la
Kimani ambacho mpaka sasa hakijakamilisha usajili wake na kupewa hati
wakati kilinunuliwa na shirika hilo mwaka 2012.
Kiwanja hicho kimejengwa nyumba za watumishi ambao wangekuwa wakifanya kazi katika kituo cha Kisarawe lakini hazijakamilika.
“Natoa
siku saba, mtu huyu awe amenipa maelezo ya kutosha kwa nini hati hiyo
imesainiwa na mtu mmoja ambaye ni yeye na ameandika jina lake badala ya
jina la Shirika, ina maana alikuwa hajui? Hii ni makusudi,” alisema Wambura.
Wambura
alisema mtu huyo amefanya makusudi kwa nafasi yake kushindwa kutambua
kukaa miaka yote hiyo bila kupewa hati na kutelekezwa bila kuendelezwa
ni ufisadi ambao hauwezi kuvumiliwa.
Awali
Wambura alipokuwa akipokea taarifa kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa
wilaya hiyo, Mwanamvua Mrindoko, alisema kiwanja hicho chenye meta za
mraba 9,567 kilipimwa na kusajiliwa kwa namba 68,480 mwaka huo huo
shirika liliomba kuandaliwa hati.
Mrindoko
alisema utaratibu wa ukamilishaji hati ulifanyika na walilipia na
kujaza fomu ya maombi ya hati. Ilielezwa kwamba, baada ya TBC kuisaini
na kuirudisha Wizara ya Ardhi ilionekana kuwa na upungufu ikarudishwa.
Alitaja
upungufu huo kuwa ni hakukuwa na nakala halisi ya kuanzishwa shirika na
pia fomu hiyo ilisainiwa na mtu mmoja badala ya wahusika wawili wa TBC
na hivyo kukwamisha mchakato wa kupata hati.
Naibu
Waziri huyo alipomhoji Ofisa miradi wa wizara hiyo, Macksselin Chota
ambaye alikuwepo kwenye ziara, alisema maelezo hayo ni sahihi na kwamba
upungufu wanaufanyia kazi. Chota alisema viwanja vingi vya TBC
havijapata hati.
Kati
ya viwanja 55, viwanja 19 pekee ndivyo vyenye hati. Alisema pia viwanja
vingi viko katika migogoro mbalimbali kama vile uvamizi na pia uporaji.
Naibu Waziri Wambura aliagiza ndani ya siku hizo saba hati ya kiwanja
hicho cha Kisarawe iwe imepatikana.
Alitaka shirika pia lieleze ni namna gani watafanya kuendeleza majengo ambayo yameanza kujengwa hapo.
“Hii
inatia mashaka kabisa, mnachelewesha kupata hati na baadaye viwanja
vinaingia kwenye migogoro, unafanya hivyo ili baadaye nyie wenyewe
mzunguke, tutashindwaje kuamini hivyo?” Alihoji Naibu Waziri.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini