MaliI
zenye thamani ya Sh bilioni sita za baadhi ya wadaiwa 16, waliokwepa
kulipa kodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), baada ya kutorosha
kontena za mizigo yao kwenye Bandari Kavu (ICD) ya Azam mwishoni mwa
mwaka jana, zimekamatwa jana na zinafilisiwa.
Aidha,
mali nyingine za thamani ya Sh bilioni 7.4 zimebainishwa na muda wowote
kuanzia leo zitakamatwa ili kufilisiwa kwa lengo la kulipa kodi
inayodaiwa na TRA.
Hayo
yalibainishwa Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya
Udalali ya Yono, iliyopewa kazi ya kufuatilia wadaiwa hao, Yono Kevella
alipokuwa akizungumzia kuanza kwa kazi ya kukamata mali za wadaiwa hao
na kufilisiwa.
Kevela
alisema baada ya kuisha muda wa siku 14, walioutoa kwa wadaiwa 24
kulipa madeni yao ya Sh bilioni 18.95, hadi juzi ni wadaiwa nane tu
waliweza kulipa, hivyo hao 16 hawakulipa na mali zao ndio zimeanza
kukamatwa na kufilisiwa.
Aliwataja
wadaiwa ambao mali zao zimekamatwa na wamekubali wenyewe zifilisiwe
kulipa deni hilo kuwa ni Tifo Global Trading Co Ltd wanaodaiwa Sh
bilioni 1.57 na Lotai Steel Tanzania Ltd wanaodaiwa Sh bilioni 5.47.
Alisema wadaiwa hao ni wawekezaji kutoka China na wamekubali kwa hiari yao mali zao zifilisiwe kulipa deni wanalodaiwa.
Mali zilizokamatwa na ziko tayari chini ya kampuni hiyo ya Yono ni kontena tisa za mabati, zenye thamani ya Sh bilioni sita.
"Nitumie
fursa hii kuwaalika wananchi wote wanaohitaji mabati waje ofisi za
kampuni yetu kununua mabati hayo, yako mengi ni kontena tisa,
tunachofanya si kumuonea mtu, bali tunatekeleza wajibu wetu tuliopewa wa
kuhakikisha kodi ya serikali inalipwa”, alisema Kevella.
Alisema
kazi ya kukamata mali za wadaiwa wengine 14, zinaendelea na ndani ya
wiki moja kazi hiyo itakuwa imekamilika na iwapo wahusika wote
hawatapatikana, Kampuni ya SSB ambayo ndiyo mmiliki wa bandari kavu ya
(Azam ICD) na kampuni ya wakala wa forodha ya Regional Cargo Services,
watahusika kulipa deni linalobaki.
"Kwa
wale tutakaoshindwa kuwapata au kukamata mali za kutosha kulipa deni
wanalodaiwa, mmiliki wa bandari kavu ya Azam ICD, na kampuni ya wakala
wa forodha ya Regional Cargo Services, watapaswa kulipa”, alisisitiza Kevella.
Kevella
alisema jana jioni walitarajia kukamata mali nyingine za Sh bilioni 7.4
za mdaiwa Tuff Tyres General Co Ltd, ambaye amekimbilia kufungua ombi
mahakamani lakini Mahakama haijatoa uamuzi.
Alisema
wameshazibainisha mali za mdaiwa huyo, ikiwa ni pamoja na jengo la
ghorofa, matairi na nyumba iliyopo Msasani, ambazo zote kwa pamoja
zikifilisiwa zitalipa deni la Sh bilioni 7.4 anazodaiwa.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini