Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia
salamu za rambirambi Mkuu wa Jeshi la Polisi hapa Nchini IGP Ernest
Mangu kufuatia kifo cha msaidizi wake Inspekta - Gerald Ryoba
aliyepoteza maisha katika ajali ya kusombwa na mafuriko ya maji wakati
akikatiza katika eneo la Kibaigwa, Wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma.
Katika
ajali hiyo iliyotokea 03 Januari, 2016 Inspekta Ryoba akiwa na Mkewe na
watoto wake wawili, pamoja na watu wengine wawili walikua wakisafiri
kutoka Geita kuja Jijini Dar es salaam na walipofika katika eneo la
Bwawani gari walilokuwa wakisafiria kusombwa na maji na wote sita
kupoteza maisha.
Rais
Magufuli amempa pole nyingi Mkuu wa Jeshi la Polisi kwa msiba huo
mkubwa, na amemuomba amfikishie salamu za pole kwa familia ya Marehemu
Ryoba na kueleza kwamba anaungana nayo katika kipindi hiki kigumu.
"Nimesikitishwa sana na tukio hili la kuondokewa na msadizi wako pamoja na familia yake, ni tukio linalotia uchungu mkubwa" amesema Mheshimiwa Rais.
Aidha,
Rais Magufuli amemuomba Mwenyezi Mungu awape nguvu na uvumilivu wafiwa
wote, na aziweke roho za marehemu mahali pema peponi Amina.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
06 Januari, 2016
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini