Rais John Magufuli amemaliza mgogoro wa ardhi baina ya wananchi wa Kapunga na mwekezaji wa Kapunga Rice Project Limited na sasa hekta 1,780 zitakuwa mali ya wananchi.
Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alitangaza jana
katika mkutano wa hadhara ambao licha ya mvua kubwa, wananchi
walimsikiliza kwa makini na kushangilia baada ya kupokea taarifa hiyo.
Kijiji cha Kapunga kina wananchi 4,500.
Lukuvi alisema hatua hiyo ni zawadi ya kwanza ya Rais kwa wananchi Tanzania kwa kutatua mgogoro wa siku nyingi.
“Rais
amedhamiria kuwasaidia wananchi, hivyo naomba (Mkuu wa Mkoa), uandae
orodha ya watu wote wanaomiliki mashamba yasiyoendelezwa ingawa wanapata
mikopo kupitia hati za mashamba hayo ili kazi ya Serikali kuwapatia
maeneo ya kulima na wananchi wa kawaida iweze kufanikiwa,” alisema.
Lukuvi
alikwenda kwenye kijiji hicho kutangaza jambo ambalo aliyekuwa waziri
wa wizara hiyo, Profesa Anna Tibaijuka alilishindwa Januari 7, 2013.
Meneja
wa Mradi Kapunga Rice Project, Sumil Tayic alisema viongozi wake
wameafiki uamuzi wa Rais bila kinyongo na sasa wataimarisha ushirikiano
mzuri na wananchi.
Mwakilishi
wa wananchi, Sekela Sandube aliishukuru Serikali hususan Rais Magufuli
na Waziri Lukuvi kwa kumaliza mgogoro ambao uliwashinda wengi kwa sababu
za roho mbaya.
Mwenyekiti
wa Kijiji cha Kapunga, Brighton Mwinuka alisema hatua ya Rais Magufuli
kuwapatia eneo hilo kutakifanya kijiji kiwe na mipango ya maendeleo.
Kabla
ya kwenda wilayani Mbarali jana, Lukuvi alikutana na Kamati ya Ulinzi
na Usalama ya Mkoa wa Mbeya kuanzia saa 2.24 hadi saa 3.57 kwenye Ofisi
ya Mkuu wa Mkoa.
Habari
kutoka kwenye kikao hicho zilisema waziri aliwaeleza kinagaubaga kuhusu
msimamo wa Serikali ya Awamu ya Tano katika kutatua kero za wananchi na
kwamba lazima viongozi wote wabadilike kiutendaji.
Alipoulizwa kilichozungumzwa Waziri Lukuvi alisema yalizungumzwa mambo mengi ya kiutendaji na baadhi angeyatoa Kapunga.
Mgogoro wa Kapunga
Mwaka
1995, wanakijiji walitoa hekta 5,500 za ardhi kwa Kampuni ya Taifa ya
Kilimo (Nafco), huku eneo la hekta 1,870 likiwa la wakulima wa kawaida.
Lakini
katika mazingira ya kutatanisha, Serikali ilichukua hati moja
iliyojumuisha hekta 5,500 na nyingine 1,870 bila kuwajulisha wananchi,
hivyo mwekezaji aliponunua eneo la Nafco alikabidhiwa hati ya eneo lote.
Serikali
ilibaini kwamba Nafco ilisajili na kupata hati moja kwa eneo lote
likiwamo la kijiji lakini kwa miaka yote imeshindwa kutoa uamuzi.
Mwaka
2013, mwekezaji huyo alidaiwa kumwaga sumu kwenye mashamba ya mpunga
yaliyokuwa na mgogoro na Serikali ilimtuma Profesa Tibaijuka
kuulimaliza.
Alifika
akiwa na msimamo wa kutaka kumshauri Rais wa Awamu ya Nne afute hati ya
eneo linalozidi ambalo ni hekta 1,870, lakini baada ya kupata maelezo
kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji, Justin Vermaak alisema anawashangaa
wananchi kudai kwa nguvu eneo ambalo ni la mwekezaji kisheria.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini