WATU wawili, baba na mwanawe wamekufa baada ya kushambuliwa na kujeruhiwa na simba mkoani Katavi.
Tukio
hilo lilijiri Januari 3, mwaka huu, pale mkazi wa kijiji cha Sitalike
wilayani Nsimbo Wilaya ya Mlele, John Jeremiah (45) na mwanawe mwenye
umri wa miaka mitano, walipouawa na simba baada ya kuwavamia wakiwa
wamelala ndani ya nyumba yao.
Akizungumzia
tukio hilo, Mwenyekiti wa kijiji hicho, Christopher Anjelo alisema kuwa
kutokana na mlango wa nyumba waliyokuwa wakiishi kutokuwa imara, simba
huyo aliuparamia, akausukuma na kuingia ndani.
Inadaiwa
kuwa simba huyo baada ya kumjeruhi vibaya na kumsababishia kifo
Jeremiah alimvamia mtoto wake na kula kiwiliwili chake ambapo alibakiza
kichwa kisha akaondoka na kutokomea porini. Kijiji cha Sitalike
kinapakana na Hifadhi ya Taifa ya Katavi iliyopo wilayani Mlele.
Mwenyekiti
wa kijiji hicho, Anjelo alitoa taarifa kwa askari wa wanyamapori wa
Hifadhi ya Taifa ya Katavi ambapo walianza kumsaka simba huyo
wakishirikiana na wananchi. Walifanikiwa kumuua simba huyo.
Inaelezwa
kuwa baada ya kumuua simba huyo, baadhi ya wakazi wa kijiji hicho
walitaka wapewe mzoga wa mnyama huyo kwa ajili ya kitoweo huku wengine
wakidai viungo vyake ni tiba za kijadi na mazindiko, lakini askari hao
wa wanyama pori walikataa na kuondoka na mzoga wa mnyama huyo kwa madai
kuwa wanenda kuuteketeza kwa moto.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini