==> Hili ni Tamko La Saed Kubenea(mbunge wa ubungo) kupangua Tuhuma Mbalimbali zilizoelekezwa kwake
NIMESOMA andishi la anayejiita Seif Rashid, lililochapishwa kwenye mitandao kadhaa ya kijamii, pamoja na baadhi ya magazeti.
Andishi
limejielekeza katika kunijadili binafsi: Jinsi nilivyofanikiwa kuwa
mbunge wa jimbo la Ubungo, kuwa mmiliki wa kampuni ya Hali Halisi
Publishers Limited – wachapishaji wa MwanaHALISI – gazeti ambalo mimi
ndiye mtendaji wake mkuu – na mengine mengi.
Andishi hili lilipewa vichwa vya maneno tofauti, kulingana na mahitaji ya mchapishaji.
Kuna
baadhi ya maeneo lilipewa kichwa cha maneno, “Saed Kubenea:
Ndumilakuwili mbobezi.” Pengine ililiandikwa, “Mfahamu Saed Kubenea,
mbunge wa Ubungo.”
Kote
lilikochapishwa andishi lile, lilibeba aya kadhaa kutoka kwenye makala
niliyoandika na kuchapishwa katika gazeti la MAWIO, toleo la Alhamisi ya
24 Desemba 2015.
Makala katika MAWIO ilikuwa inajadili ndimi mbili za Kiongozi Mkuu wa ACT- Wazalendo, Zitto Zuberi Kabwe.
Mwandishi
anasema, nimeamua kumshambulia Zitto, kwa sababu nataka kuwa Mwenyekiti
wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ambayo Zitto pia
anaitaka tena.
==>Baada ya kuisoma na kuirejea tena na tena, napenda kueleza yafuatayo:
Ni
kweli kwamba Saed Kubenea ndilo jina langu. Ni kweli kuwa mimi ni
mbunge wa Ubungo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Ni
kweli kwamba niliwahi kuandikia magazeti ya Mtanzania na RAI – hakuna
lisilo la kweli. Basi. Yaliyobaki katika andishi la anayejiita Seif
Rashid, ni uongo wa moja kwa moja, porojo au tuhuma zenye nia ya
kunidhalilisha na kunivunja moyo.
Niseme
hapa mapema kuwa, mimi siyo mtu wa kuvunjika moyo pale ninapokuwa
nimeamua kufanya jambo. Mimi sitishwi na uongo, uzushi, porojo au suto
za kwenye magenge ya kahawa au bao.
Alichokifanya anayejiita Seif Rashid, ni kuokoteza huku na kule na kutaka kuaminisha umma kuwa ni ukweli. Kwa mfano, sijawahi kutamka mahali kokote kuwa nataka kuwa mwenyekiti wa PAC. Spika wa Bunge hajapanga nani awe kamati hii au ile. Wala haijafahamika kuwa nitakuwa mjumbe wa kamati ipi.
Hata kama nitataka kuwa mwenyekiti, bado siwezi kutumia kalamu yangu kujipigia kampeni. Siamini katika siasa za aina hiyo.
Mwenye
andishi anasema, ninatumia cheti cha ndugu yangu aishiye Bagamoyo na
mwenye jina la Said (sio Saed); na kwamba mimi siitwi Saed Kubenea.
Hataji jina langu.
Hata
hivyo, ni vema nieleze yafuatayo: Jina la Saed Kubenea, ndiyo jina
halisi nililopewa na wazazi wangu. Nimelirithi kutoka kwa babu yangu.
Anaitwa, Saed Mohammed Kubenea. Aidha, hakuna kaka au ndugu yangu yeyote
anayeishi Bagamoyo. Hayupo.
==>Nimesoma
kwa kadri Mwenyezi Mungu alivyonisaidia. Nilimaliza Kidato cha Nne.
Nikaanza kujifunza mwenyewe na baadaye kupata msaada wa watu mahili
kunifundisha taratibu uandishi wa habari.
==>Nikahudhuria
mafunzo mafupi hapa na pale nchini. Hatimaye nikapata mafunzo ya juu ya
uandishi wa habari nchini Uholanzi na India. Ninaendelea kujifunza na
elimu haina mwisho.
Jingine
la kugusia ni madai kuwa nilihusika na upoteaji wa anachoita, “kompyuta
mpakato (laptop) ya Prof. Ibrahim Lipumba mwaka 2005.”
Suala hili liliwahi kuelezwa pia na Didas Masaburi, aliyekuwa mshindani wangu katika mbio za ubunge jimboni Ubungo.
Ukweli ni huu: Prof. Lipumba hajawahi kuibiwa kompyuta (laptop) akiwa na mimi. Kilichoibiwa
akiwa na mimi ni modemu inayotumika kwa ajili ya kupata huduma ya
intaneti. Bali kompyuta inayodaiwa kuwa ya Prof. Lipumba ilikuwa ni mali
yangu. Siyo ya Prof. Lipumba kama ambavyo wahusika wanataka kuaminisha
umma.
Kuna hili la gazeti la Hali Halisi ambalo mwandishi anasema, nilipewa mtaji na Prof. Lipumba
na baadaye likatumika kama gazeti rasmi la kambi ya upinzani bungeni.
Mimi sikuanzisha gazeti hili. Lilianzishwa na wabunge wa upinzani mwaka
2003. Kiongozi wa Kambi ya Upinzani alikuwa Willifred Lwakatare, mbunge
wa Bukoba Mjini wakati huo.
Ninashangaa
mtuhumu anapopata taarifa kwamba kufa kwa gazeti la Hali Halisi,
kulinifanya kuwa na maisha magumu; na kwamba kwa huruma, Zitto Kabwe na mwenzake, Halima Mdee, wakanipa mtaji wa kuanzisha gazeti la MwanaHALISI. Hii siyo kweli na aliyeandika hivyo anajua si kweli.
Kampuni
ya Hali Halisi Publishers Limited ilianzishwa 31 Januari 2005. Wakati
huo Zitto na Mdee hawakuwa wabunge. Zitto na Halima hawakushiriki kwa
namna yoyote ile katika kuanzisha gazeti hili. Mdee akiulizwa juu ya
hili ataeleza. Hata Zitto anajua vema; na akiwa mkweli, atasema
hivyohivyo. Historia isipotoshwe.
Gazeti
la MwanaHALISI limeanzishwa na mimi kwa ushirikiano mkubwa kutoka kwa
Absalom Kibanda na baadhi ya waandishi wengine mahiri. Labda niseme
hivi, kwamba anayetaka kujua historia yangu, ya vyombo vyangu vya habari
na maisha yangu ya mapambano; afanye ahadi na mimi, tukae, aniulize,
nimweleze ili apate ukweli na usahihi juu yangu na kazi yangu, na hata
ubunge wangu.
Hebu niweke wazi jambo hili: Kwanza, sijawahi kuwa na urafiki, kwa maana halisi ya urafiki, na Zitto. Kilichokuwepo ni ukaribu tu kama ilivyo kwa watu wengine mnapokuwa pamoja.
Pili, sishindani na Zitto.
Katika lipi? Kila mmoja ana taaluma yake; na taaluma hizi zaweza
kufanya kazi nzuri na vizuri kama hakutakuwa na unafiki, uzandiki na
undumila kuwili kama nilioueleza katika makala yangu.
Tatu, siamini katika kuomba fadhila na kujikomba. Naamini
katika kudai haki na kilichochangu; au ninachostahili kwa mujibu wa
taratibu, kanuni, sheria na katiba. Haya hayahitahi kujikomba.
Yanahitaji ujasiri na moyo wa utumishi kwa umma. Huko ndiko kwangu.,.
Monday, January 4, 2016
Saed Kubenea Akana Tuhuma Dhidi Yake.....Asimulia Jinsi Alivyosoma, Akana Kuiba Laptop ya Prof. Lipumba
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini