Hatimaye,
Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad
ametoa msimamo wake na chama chake kufuatia mazungumzo ya siri ya
kutafuta suluhu ya mkwamo wa kisiasa unaotokana na tangazo la kufutwa
kwa uchaguzi wa Zanzibar.
Akizungumza
leo na waandishi wa habari katika hotel ya kitalii ya Serena jijini Dar
es Salaam, Maalim Seif amesisitiza kuwa hoja ya kurudia uchaguzi wa
Zanzibar kama inavyoelezwa na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),
haina msingi, haikubaliki na sio halali kikatiba.
“Hoja
ya kurudia uchaguzi haina msingi, haina uhalali, ni hoja ambayo inaweza
kuzaa fujo na vurugu na inaweza kuleta mzozo mkubwa wa kikatiba wa
kisheria. Sidhani kama tunataka kuwapeleka huko watanzania,” alisema Maalim Seif.
Makamu
huyo wa kwanza wa rais wa Zanzibar ameeleza kuwa tayari wameshafanya
vikao nane vilivyowashirikisha wagombea urais pamoja na marais wastaafu
wa Zanzibar lakini hawakukubaliana kurudia uchaguzi kama baadhi ya
viongozi wa CCM walivyoeleza.
Aidha,
Maalim Seif amekanusha kilichoelezwa na Makamu wa Pili wa Rais Balozi
Seif Ali Idd baada ya kukutana na Rais John Magufuli, kuwa rais alisema
warudie Zanzibar kujiandaa na marudio ya uchaguzi kwani rais hakusema
hivyo alipokutana naye.
Maalim
Seif amesema kuwa ana imani kubwa na rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Dk. John Magufuli katika kuleta maridhiano na ufumbuzi wa
mgogoro wa Zanzibar kutokana na mazungumzo aliyofanya naye hivi karibuni
katika Ikulu ya Magogoni jijini Dar es Salaam.
Amesema
kuwa endapo uchaguzi mkuu utatakiwa kurudiwa, zipo changamoto nyingi za
kikatiba ambazo zitakwamisha zoezi hilo hivyo uchaguzi huo
hautawezekana.
Ametaja
changamoto hizo kuwa ni pamoja na kupitishwa kwa fedha za kugharamia
uchaguzi na baraza la wawakilishi ambalo hivi sasa halipo kwa kuwa
limefikia ukomo wake.
Mbali
na hilo, Maalim Seif alieleza kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi
(ZEC), Jecha Salum Jecha anapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria na
kinidhamu kwa kutoa tamko lisilo halali la kufuta uchaguzi huo huku
akifahamu dhahiri kuwa hana nguvu hiyo kikatiba.
Ameitaka
ZEC iongozwe na makamu mwenyekiti wake kwa mujibu wa katiba pamoja na
wajumbe wengine kukamilisha utaratibu wa kuhakiki matokeo ya uchaguzi na
kumtangaza mshindi.
Maalim
Seif ameeleza kuwa anafahamu dhahiri kuwa kuna mpango wa kutangaza kwa
nguvu marudio ya uchaguzi Februari 28 mwaka huu, lakini yeye pamoja na
chama chake hawatakubali.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini