Mashirika
ya dini ni miongoni mwa taasisi zilizotakiwa kuwasilisha nyaraka kwa
ajili ya kuhakiki kama yalilipa ushuru wa bandari uliosababisha Serikali
kupoteza Sh48 bilioni.
Uwapo
wa taasisi hizo za kiimani kwenye sakata hilo ulibainishwa jana katika
orodha ya iliyotangazwa jana na Mamlaka ya Bandari (TPA) ambayo ina
kampuni na taasisi 40 zaidi ya orodha iliyotangazwa juzi yenye kampuni
243. Kwa tangazo la jana, kampuni na taasisi zinazotakiwa kuwasilisha
nyaraka kuhusu malipo hayo sasa ni 283.
Tangazo
la TPA lilitolewa jana likiwa na tarehe ya Desemba 24, linazitaka
taasisi hizo ambazo ni Baraza la Kikristo Tanzania (CCT) na Shirika la
Misaada la Kanisa Katoliki, Caritas Tanzania na nyingine 281 kwenda
kuchukua barua zao kwa ajili ya uhakiki wa malipo ya ushuru huo
yaliyofanyika kuanzia Julai 2014 hadi Aprili, 2015.
Taasisi
nyingine maarufu zilizopo katika orodha hiyo ni klabu maarufu ya mchezo
wa soka ya Azam Football, kampuni maarufu ya Toyota Tanzania Ltd na
Bakhresa Food Products.
Juzi
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa
alizihusisha baadhi ya taasisi hizo 283 na upitishaji wa makontena
11,884 na magari 2,019 kwenye bandari bila kulipia ushuru wa bandari.
Kubainika
kwa ukwepaji huo ushuru, kunafanya idadi ya makontena yaliyohusika
katika suala hilo kufikia 14,664. Awali makontena 349 yaligundulika
kupitishwa kinyemela baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufanya ziara
bandarini na mengine 2,431 kubainika baadaye.
Mbarawa
aliwataka mawakala wa forodha na kampuni hizo 283 zinazotuhumiwa katika
utoaji wa makotena na magari bila kulipia ushuru kupeleka vielelezo vya
uthibitisho ndani ya siku saba kuanzia juzi.
Msemaji wa CCT, Mchungaji John Kamoyo alisema watafanya kama lilivyoagiza kwenda kuchukua barua zao.
“Kama walivyoeleza sisi tutaenda kuchukua barua na kufahamu kilichopo ndani na tutafanya kama walivyoagiza,” alisema Kamoyo huku akikataa kuhusisha wito huo na suala lolote linalohusina na ukwepaji wa kodi.
Katibu mtendaji wa Caritas Tanzania, Laurent Masui alisema atashirikiana na mamlaka hiyo kutimiza agizo hilo.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini