Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe Dkt. John Pombe Magufuli
ameagiza waliokuwa wakazi wa Magomeni Kota kukaa kwenye nyumba za
Serikali miaka mitano bure na baadaye kuzinunua kwa bei nafuu.
Rais Magufuli ameyasema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akiwahutubia wakazi wa Magomeni na kuagiza ujenzi wa nyumba hizo kuanza ndani ya miezi miwili.
“Nasema
wakandarasi ndani ya miezi miwili waanze kujenga nyumba 644 kwa ajili
ya wazee ambao wameteseka sana baada ya nyumba zao kuvunjwa, nitatoa
fedha Serikalini mwezi huu kwa ajili ya kuanza kwa shughuli hiyo”
alisema Dkt. Magufuli.
Ameongeza
kusema kuwa ujenzi huu anataka ukamilike ndani ya mwaka mmoja au miezi
sita kama ulivyokuwa kwa hosteli za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Rais Magufuli amesema atafurahi kukabidhi hati kwa wakazi wa Magomeni Kota pindi nyumba hizo zitakapokuwa zimekamilika.
“Namuomba Mwenyezi Mungu anipe uzima ili nyumba hizo zikiwa tayari hati nizikabidhi mwenyewe,”alisema Magufuli.
Rais
Magufuli ameonyesha kukerwa na vitendo vya baadhi ya watumishi wa
Serikali wasio waaminifu kuwanyima haki wanyonge. Amesema vitendo hivyo
vya unyanyasaji viishe mara moja na watanzania wakae kwenye nchi yao kwa
amani.
Aidha,
Rais Magufuli amemwagiza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa
(NHC), Nehemia Mchechu kukusanya madeni yote ya kodi kwa wanaodaiwa na
shirika hilo bila kujali chama, serikali au mtu yeyote.
Ameagiza kuwa wanaodaiwa inabidi walipe deni lao ndani ya siku 7 (saba) vinginevyo waondolewe kwenye nyumba hizo.
Kwa
upande wake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe.
William Lukuvi amemshukuru Rais Magufuli kwa kuwajali wanyonge hasa kwa
kutatua mgogoro wa makazi kwa wakazi wa Magomeni Kota.
“Mheshimiwa
Rais ninakushukuru kwa kuwajali wazee hawa wa Magomeni, nami
nilitekeleza maagizo yako na kufuatilia mgogoro huu hadi kupata
ufumbuzi”, alisema Lukuvi.
Lukuvi
amesema kuwa mgogoro wa Magomeni ulivyokuwa mkubwa ulistahili nguvu ya
Mhe. Rais Magufuli, lakini kwa migogoro mingine ambayo ni midogo, hiyo
ameishughulikia na ataendelea kuishughulikia ili kero za wananchi kuhusu
ardhi ziishe kama alivyoagizwa na Rais.
Nyumba
zilizokuwa Magomeni Kota zilivunjwa mwaka 2009 na wananchi wakaahidiwa
kujengewa nyumba ambazo wangeuziwa kwa bei nafuu. Lakini kwa takribani
miaka mitano nyumba hizo hazikujengwa hali ambayo iliwafanya wakazi hao
waishi maisha ya kuangaika.
Hivi
karibuni Mhe. Rais John Pombe Magufuli alifuta hati zote za umiliki
eneo la Magomeni Kota na kuondoa usimamizi wa Nyumba TAMISEMI na
kuupeleka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya
kuanza kusimamia ujenzi.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akipeana
mikono na Mwenyekiti wa waliokuwa wakaazi wa nyumba za Magomeni Kota
Bw. George Abdi wakati alipotembelea na kuongea na wakaazi hao wa
Magomeni Kota jijini Dar es salaam leo Septemba 6, 2016.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akimfariji
Bi. Mwajuma Sama kwa taabu walizopata yeye kiongozi na wakaazi
wenzie wa Magomeni Kota jijini Dar es salaam leo Septemba 6, 2016.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli akimshukuru
wakili Twaha Taslima wa Law Chambers kwa kusimamia vyema maswala ya
mgogoro wa eneo iliyokuwa Magomeni Kota jijini Dar es salaam leo
Septemba 6, 2016. PICHA NA IKULU
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini