Serikali
imekataa kuongeza fedha za kujikimu kwa wanafunzi wa elimu ya juu
wanaopatiwa mikopo na Serikali kutoka Sh8,500 hadi kufikia Sh10,000 kwa
siku.
Naibu
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Stella Manyanya amelieleza
Bunge kuwa kiwango hicho kitaendelea hadi utakapofanyika utafiti baada
ya miaka miwili.
Manyanya
alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Zainabu Katimba (CCM),
aliyetaka kujua kama Serikali itakuwa tayari kuongeza fedha kwa
wanafunzi hadi kufikia Sh 10,000 kwa madai gharama za maisha zimepanda.
Amesema
bodi ya mikopo ilifanya ongezeko la fedha za kujikimu kwa wanafunzi wa
vyuo vikuu kwa Sh1,000 kutoka Sh7,500 hadi kufikia 8,500 katika mwaka
2015/16.
“Ongezeko
hilo haliendani na kasi ya mfumuko wa bei uliorekodiwa na Ofisi ya
Taifa ya Takwimu (NBS) kutoka asilimia 4.2 Februari 2015 hadi kufikia
asilimia 5.6 Februari 2016,” amesema Katimba.
Naibu
waziri amesema Serikali imekuwa ikifanya utafiti wa gharama halisi za
maisha kwa wanafunzi ambazo hujumuisha malazi na chakula.
Amesema
katika mwaka wa fedha wa 2014/15 Serikali kupitia bodi hiyo ilifanya
utafiti katika vyuo vyote nchini ili kujua gharama halisi za chakula na
malazi na kuonyesha kuwa gharama halisi ilikuwa ni kati ya Sh8,000 hadi
8,500.
Naibu
waziri amesema wizara itafanya utafiti mwingine ili kubaini gharama
halisi za chakula na malazi kwa wanafunzi hao na matokeo yake yatatumika
kupanga viwango vya fedha zitazolipwa kwa wanafunzi.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini