Rais
wa Jamhuri ya Sudan Kusini Mhe. Salva Kiir Mayardit amemtumia ujumbe
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ambaye
pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki akimuarifu kuwa hali ya
usalama katika nchi hiyo imeanza kutengemaa.
Rais
Salva Kiir Mayardit amewasilisha ujumbe huo kupitia kwa Mjumbe wake
Maalum Mhe. Aggrey Tisa Sabuni ambaye pamoja na kuwasilisha ujumbe huo
amesema Sudani Kusini imekamilisha nyaraka za azimio la kuridia mkataba
wa kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao umewasilishwa jana
tarehe 05 Septemba, 2016 katika makao makuu ya Jumuiya Jijini Arusha.
Mhe.
Aggrey Tisa Sabuni amesema Sudan Kusini ipo tayari kushirikiana na nchi
wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika masuala mbalimbali
yenye manufaa kwa wananchi ikiwemo biashara na uwekezaji na kwamba ni
matumaini yake kuwa itapata ushirikiano mzuri.
Kwa
upande wake Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa kwake na taarifa za
kutengemaa kwa hali ya amani nchini humo na kwamba ni matarajio yake
kuwa Sudan Kusini itajikita katika maendeleo ya wananchi wananchi wake.
Katika
hatua nyingine, Rais Magufuli amepokea ujumbe kutoka kwa Rais wa
Jamhuri ya Burundi Mhe. Pierre Nkurunziza ulioletwa na Mjumbe Maalum wa
Rais huyo Mhe. Aime Laurentine Kanyana.
Katika
ujumbe huo Rais Nkurunziza amesema hali ya Burundi ni shwari na kwamba
wananchi wa Burundi wanaendelea na shughuli zao kama kawaida.
Kwa
upande wake Rais Magufuli amesema Tanzania yenye wakimbizi takribani
200,000 wa kutoka Burundi inafurahishwa na taarifa za kuwepo hali ya
amani nchini humo.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
06 Septemba, 2016
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini