Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amewasihi
wananchi wa Kisiwa cha Pemba kutokubali kurubuniwa na watu
wanaowachochea kufanya vitendo vya uvunjifu wa amani kwa kuwa vitendo
hivyo vinarudisha nyuma juhudi za kuwaletea maendeleo na kutatua kero
zinazowakabili.
Rais
Magufuli amesema hayo tarehe 02 Septemba, 2016 wakati akihutubia
Mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Gombani ya Kale Wilaya
ya Chakechake Mkoani Kusini Pemba, ambao umehudhuriwa na Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein.
Rais
Magufuli amesema Kisiwa cha Pemba kina fursa nyingi za maendeleo
ikiwemo Uvuvi wa baharini, Utalii na Kilimo lakini endapo wananchi
wataendelea kushabikia uchochezi na vitendo vya kuvuruga amani
vinavyofanywa na baadhi ya watu, hakuna mwekezaji atakayekuwa tayari
kuwekeza.
""Hawezi
akaja mtu kujenga kiwanda wakati hakuna amani, sisi vijana lazima tuwe
mstari wa mbele kujenga amani ili wawekezaji waje wajenge viwanda na
tupate ajira.
"Hapa
Pemba kuna fukwe nzuri ambazo zinafaa kujenga hoteli kubwa za kitalii,
nani atakuja kujenga hoteli kama hakuna amani?" Amehoji Rais Magufuli
huku akisisitiza kuwa umefika wakati kwa wananchi wa Pemba kubadilika na
kujikita katika masuala ya maendeleo.
Hata
hivyo Rais Magufuli ameonya kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania haitawafumbia macho watu wanaofanya uchochezi unaolenga
kuvuruga amani na ameviagiza vyombo vya dola vianze kuwafuatilia wote
walioanza kufanya uchochezi huo.
Amesisitiza kuwa uchaguzi umekwisha na kilichobaki sasa ni kwa watanzania kufanya kazi na kujenga nchi yao.
Mapema
akimkaribisha Rais Magufuli kuzungumza na wananchi hao, Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein
amewaambia wananchi wa Zanzibar kuwa tangu aingie madarakani yeye na
Rais Magufuli wamefanya mambo mengi kwa manufaa ya Watanzania
Dkt.
Shein ameongeza kuwa hali ya Muungano ni nzuri na kwamba sehemu kubwa
ya kero za Muungano zimetatuliwa huku akibainisha kuwa kwa sasa kazi
iliyopo ni kutafuta changamoto mpya za Muungano zenye lengo la kuchochea
maendeleo.
Mkutano
huo umehudhuriwa na Mke wa Rais Magufuli Mama Janeth Magufuli na Mke wa
Rais Shein, Mama Mwanamwema Shein, Mawaziri na viongozi mbalimbali wa
Siasa, Dini na Serikali.
Jioni
hii (jana) Rais Magufuli amewasili mjini Unguja ambapo kesho tarehe 03
Septemba, 2016 ataendelea na ziara yake kwa kuzuru kaburi la Rais wa
Kwanza wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Marehemu Sheikh
Abeid Amaan Karume, kuzuru kaburi na kutoa mkono wa pole kwa familia ya
aliyekuwa Rais wa Zanzibar na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Marehemu Aboud Jumbe Mwinyi na baadaye atazungumza
na wananchi katika Mkutano wa hadhara utakaofanyika katika Uwanja wa
Demokrasia Kibandamaiti Mjini Unguja.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Unguja
02 Septemba, 2016
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini