Naibu Waziri Wa Mambo Ya Ndani Ya Nchi Afanya Ziara Gereza la Msalato – Dodoma . | nyula blog

Habari Kila Pande

Breaking News
Loading...

Sunday, May 29, 2016

Naibu Waziri Wa Mambo Ya Ndani Ya Nchi Afanya Ziara Gereza la Msalato – Dodoma .



Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni amesema Serikali imejipanga kulitumia Jeshi la Magereza kuhakikisha Tanzania inaingia kwenye uchumi wa viwanda.

Lengo hilo ni mkakati wa wizara kutaka kuendana na kauli ya Rais John Magufuli ambaye amekuwa akisisitiza kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda kuelekea kwenye uchumi wa kati ifikapo 2025.

Masauni aliyasema hayo jana alipotembelea mradi wa kiwanda cha kokoto cha Gereza la Msalato kilichopo Dodoma. Alisema Magereza ina rasilimali nyingi ambazo zikitumika kikamilifu zinaweza kuifanya nchi kupiga hatua.

 Alisema kuna fursa nyingi ambazo jeshi hilo linaweza kuzitumia kufikia azma hiyo, ikiwamo kuanzisha kiwanda cha viatu kwa ajili ya askari wa majeshi mbalimbali.

 “Inashangaza kuona majeshi yetu yananunua viatu kutoka nje wakati vinaweza kutengenezwa na Magereza. Lazima tujipange na ninaamini Jeshi la Magereza linaweza kuifanya kazi hiyo,” alisema Masauni. 

Akizungumzia mradi wa kokoto wa gereza hilo, alisema zinahitajika Sh2.5 bilioni kwa ajili ya uwekezaji katika mradi huo.

 Alisema kiwanda hicho kikianza kazi kitakuwa na uwezo wa kukusanya mapato ya Sh6.8 bilioni kwa mwaka. Alisema kuna namna mbalimbali jeshi hilo linaweza kupata mtaji huo ikiwa ni pamoja na kuomba mkopo kwenye benki za nchini, kuingia ubia na mwekezaji au kupata ruzuku kutoka serikalini.

“Nataka Magereza watafute namna ya kupata fedha hizo bila kusubiri ruzuku kutoka serikalini. Najua watapata fedha hiyo kwa sababu mradi huu ni mkubwa na utalifanya jeshi hili kuongeza mapato,” alisema.

 Masauni aliongeza kuwa anataka kuona siku moja jeshi hilo linajiendesha kwa kujitegemea kuanzia kwenye chakula cha wafungwa mpaka miundombinu yake.

Alisema hilo litawezekana kama watawekeza kwenye viwanda. Mrakibu Msaidizi wa Magereza, Patrick Nasola alisema mradi huo utaendeshwa na jeshi hilo na kuwa watakuwa tayari kumuuzia mtu yoyote kokoto watakazozalisha.

Alisema mradi huo ukianza kazi utakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 15 za kokoto kwa siku. Alisema changamoto wanayokabiliana nayo ni uhaba wa fedha kwa ajili ya kutengeneza mtambo wao ambao sasa umeharibika.

“Walikuja wataalamu katika eneo hili la Msalato kupima wakabaini kuna madini mawe mengi na sasa tuna leseni 15 kwa ajili ya madini mawe. Mawe yaliyopo hapa ni kama yale yanayotumika kutengeneza tiles,” alifafanua.

Nasola aliongeza kuwa wataweza kuzalisha fedha nyingi kutokana na mradi huo kwa sababu ni eneo kubwa ambalo kwa ujumla wake lina madini mawe ya kutosha. Alisema wanatarajia kuuza zaidi kokoto ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Msalato utakapoanza.

Kwa upande wake, Mkuu wa Gereza la Msalato, Steven Mwihambi alisema kokoto ni moja ya miradi inayofanyika katika gereza hilo.

Alitaja miradi mingine kuwa ni ufugaji, kilimo na utengenezaji wa samani. “Tutaanzisha viwanda vidogo vidogo kwa ajili ya mazao tunayozalisha kama vile alizeti. Changamoto kubwa ni uhaba wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mipango yetu,” alisema kiongozi huyo wa gereza.
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini

google+

linkedin